
Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar katika mazungumzo
kati yake na Madaktari wapya pamoja na wale wanaomaliza muda wao kutoka
Jamhuri ya Watu wa China, wakiongozwa na Balozi Mdogo wa nchi hiyo
anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Balozi Xie Xiaowu.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alieleza kuwa utamaduni wa nchi
hiyo wa kuleta Madaktari kwa ajili ya kutoa huduma za afya hapa
Zanzibar ni wa kihistoria ambao umeanza tokea mwaka 1964 na kuendelea
hadi hivi leo ambapo China ilianza kuleta wataalamu wake mbali mbali
hapa Zanzibar wakiwemo Madaktari.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na
wananchi wa Zanzibar wanathamini na wanazipenda huduma zinazotolewa na
Madaktari kutoka nchini China ambao wamekuwa wakishirikiana vyema na
Madaktari wazalendo kutoa huduma hizo kwa ufanisi mkubwa hapa Zanzibar.
Pia, Dk. Shein, alitumia fursa hiyo kueleza uhusiano na ushirikiano
uliopo kati ya China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar
huku akiahidi kuendelezwa na kudumishwa na kusisitiza kuwa China
imeweza kutoa mchango mkubwa katika mafanikio ya sekta ya afya na sekta
nyengine mbali mbali hapa Zanzibar ikiwemo sekta ya viwanda,
elimu,kilimo, michezo, habari na nyengienzo.
Dk. Shein aliwakaribisha Madaktari hao wapya hapa Zanzibar na kuwaaga
wale waliomaliza muda wao huku akieleza matumaini yake makubwa kuwa
madaktari hao wapya kuwa watafanya kazi kwa ufanisi mkubwa zaidi kama
wenzao wanao ondoka ambao wamefanya kazi vyema katika kutoa huduma za
afya.
Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Madaktari 21 wanaomaliza muda wao
kwa kusaidia kutoa huduma mbali mbali za afya ikiwa ni pamoja na kutoa
mafunzo kwa madaktari na wauguzi kwa vitendo yakiwemo mafunzo ya
upasuaji na matumizi ya mashine mpya katika hospitli ya Mnazi Mmoja
ikiwemo mashine mpya za kisasa (TURP), zikiwemo upasuaji wa matatizo ya
mkojo pamoja na tiba ya njia ya mfumo wa chakula pamoja na huduma
nyenginezo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya
Watu wa China chini ya kiongozi wake Rais Xi Jingping kwa kuendelea
kuisaidia na kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali mbali
ya maendeleo hapa Zanzibar.
Akitoa pongezi hizo, Dk. Shein alisema kuwa Rais Xi Jingping ameweza
kutekeleza makubaliano yote aliyoahidi kuisaidia Zanzibar ikiwa ni
pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee pamoja na vifaa vyake
ambao tayari umekamilika, ujenzi wa uwanja wa Maotsetung, ujenzi wa
Bandari mpya ya Mpigaduri, ujenzi wa jengo jipya la abiria katika
kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume na miradi mengineyo.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alimueleza Balozi mdogo huyo wa
China kuwa ipo haja kwa China kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
juhudi zake za kuendeleza sekta ya afya kwa kuunga mkono uendelezaji wa
kitengo cha saratani, kitengo cha maradhi ya mkojo na vigo pamoja na
uanzishwaji wa kitengo cha upasuaji wa moyo ili huduma hizo ziweze
kutolewa hapa hapa Zanzibar ambapo tayari baadhi ya huduma hizo
zimeshaanza kutolewa.
Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa juhudi ilizoanza kuchukua
Serikali katika kuviimarisha vitengo hivyo ni kutoa mafunzo kwa
madaktari wachache wa vitengo hivyo pamoja na baadhi ya vifaa lakini
hata hivyo alisisitiza haja ya kuungwa mkono ili kuongeza nafasi zaidi
za masomo kwa ajili ya madaktari na wataalamu wa kada hizo, vifaa na
mambo mengineyo hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa
katika kada hizo.
Nae Balozi Mdogo wa China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Balozi
Xie Xiaowu alimueleza Dk. Shein kuwa timu ya 26 ya Madaktari kutoka
nchini China inayomaliza muda wake imefanya kazi vyema na kuahiadi timu
ya 27 nayo itafuata nyayo hizo hizo kwa kufanya vizuri sambamba na
kuhakikisha inatoa ushirikiano mkubwa kwa wananchi, madaktari wazalendo
pamoja na viongozi wa Serikali.
Balozi Xie Xiaowu alimuhakikishia Dk. Shein kuwa China itaendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi yake ya maendeleo
sambamba na kuimarisha uchumi wake kwa kutambua kuwa nchi mbili hizo
zinaurafiki na udugu wa miaka 53 tokea Mapinduzi Matukufu ya Januari 12,
1964.
Nae kiongozi wa Madaktari hao waliomaliza muda wao, Dk. Xu Zhuoqun
alitoa pongezi kwa mashirikiano mazuri aliyoyapata kutoka kwa viongozi
wa Serikali, madaktari wazalendo pamoja na wananchi wakati wote
walipofanya kazi zao hapa Zanzibar huku wakiwasifu watu wa Zanzibar kwa
ukarimu wao mkubwa.
Nao Madaktari wapya chini ya kiongozi wao Dk. Wang Hao, walitoa
shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk.
Shein kwa makaribisho na mapokezi mazuri waliyoyapata hapa nchini na
kuahidi kutoa ushirikiano wao kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Unguja
na Pemba katika kutoa huduma ya afya.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
chanzo: zanzibar24
Comments