
Balozi Seif alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Kamanda Mpya wa
Brigedia Nyuki Zanzibar Brigedia General Fadhil Nondo aliyefika
Ofisini kwake kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa
huo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ} hivi karibuni.
Brigedia General Fadhil Nondo alikuwa akikaimu nafasi hiyo tokea
Mwezi Januari Mwaka huu wa 2017 baada ya aliyekuwa akishikilia wadhifa
huo Brigedia General Cyrill Ivor Mhaiki kufariki Dunia Mapema mwaka
huu.
Balozi Seif alisema Zanzibar inapaswa kuwa katika ulinzi wa uhakika
muda wote kulingana na mazingira yake yaliyozunguukwa na Bahari ambayo
wakati kwengine hutoa nafasi kwa wahalifu kufanya vitendo
vinavyosababisha hofu na shaka kwa Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Brigedia Kamanda
huyo wa Nyuki kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Viongozi wake
itakuwa tayari wakati wote kumpa ushirikiano wa karibu zaidi ili
kuhakikisha anatekeleza vyema dhamana aliyokabidhiwa na Taifa.
Hata hivyo katika utekelezaji wa majukumu yake Balozi Seif alimshauri
Brigedia General Fadhil Nondo kushirikiana na Makamanda na walinzi wa
Vikosi vyengine vilivyopo Zanzibar ili kazi yao ya ulinzi iende vyema
bila ya kukaribisha vikwazo, mikwaruzo au migongano yoyote ile isiyokuwa
na faida.
Balozi Seif alimtakia kheir na mafanikio katika uwajibikaji wake huo
Mpya Kiongozi huyo Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ} kwa
upande wa Visiwa vya Zanzibar.
Mapema Brigedia General Fadhil Nondo alimuahidi Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar kwamba atakuwa tayari kupokea maagizo yoyote
atakayopewa kuyatekeleza katika nafasi yake hiyo mpya ya Uongozi.
Kamanda Nondo alisema kwa mujibu wa Mfumo na Taratibu za Jeshi la
Wananchi wa Tanzania nafasi yake ya kazi inawajibika kutekelezwa kwa
kupokea maagizo na ushauri kutoka kwa Viongozi wa Juu wa eneo
analofanyia Kazi.
Brigedia General Fadhil Nondo kabla ya uteuzi huo alikuwa Afisa
Mafunzo na Operesheni wa Brigedia Nyuki pamoja na Mkuu wa Kambi la JWTZ
iliyopo Bavuai Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.
![]() |
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/6/2017.
chanzo: zanzibar24.
Comments