Wizara ya Ujenzi yapanga kutekeleza vipaumbele vyake 2017/2018.

baraza-la-wawakilishiWizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji imesema katika mwaka wa Fedha 2017/2018 imepanga kutekeleza vipaumbele  vyake ikiwemo kuimarisha na kuboresha huduma za makaazi, mawasiliano pamoja na usafirishaji.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi  ya Fedha kwa mwaka 2017/2018  katika kikao cha baraza la wawakilishi Waziri wa wizara hiyo Balozi Ali Adeid Karume amesema  kipaumbele hicho  kimepanga  kuanza ujenzi wa barabara ya bububu, mahonda hadi mkokotoni yenye urefu wa 31.


Aidha amesema mbali na barabara hiyo kipaumbele hicho pia kitajenga barabara ya koani jumbi yenye urefu wa kilomita 6.3, ujenzi wa barabara ya wete chake yenye urefu wa kilomita 22 pamoja na ujenzi wa barabara ya ole kengeje yenye urefu wa kilomita 35.

Hata hivyo amesema katika kuzitekeleza ahadi za Rais wa Zanzibar juu ya ujenzi wa barabara mbalimbali  kipaumbele hicho pia kimekusudia kutengeneza madaraja yote yaliyoathirika na mvua za masika ikiwemo changaweni,kiwani,kuugoni,mwanakwerekwe,pujini,kipapo na kibonde mzungu.

Akizungumzia sekta ya Usafirishaji Balozi Karume amesema Serikali imekusudia kununua meli mpya mbili za mafuta na abiria na boti ndogo za kusafirishia abiria katika maeneo ya visiwa vidogo vidogo ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa usafiri wanaokaa visiwani humo.

Sambamba na hayo amesema wizara itahakikisha inaimarisha ulinzi na usalama wa baharini kwa kununua boti nne za doria ambazo zitafanya kazi kwenye ukanda wa pwani wa Zanzibar kwa lengo la kuwadhibiti wahalifu hususani waingizaji wa biashara za magendo.
chanzo: Zanzibar24

Comments