Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amenunua hisa za kampuni ya Vodacom Tanzania Plc zenye thamani ya Sh 10 milioni pamoja na nyingine za Sh 10 milioni kwa ajili ya mke wake, Mary Majaliwa.
Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo leo hii (Ijumaa, Mei 5, 2017) wakati akizungumza na waandishi wa habari mbele ya wakuu wa Masoko ya Hisa na Dhamana; Soko la Hisa la Dar es Salaam, viongozi wa Baraza la Uwezeshaji na kampuni ya Vodacom katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amewasihi Watanzania walioko ndani na nje ya nchi wachangamkie fursa ya kununua hisa hizo ili waweze kuwa wamiliki wa kampuni kupitia hisa zao.
“Hii ni fursa kwa Watanzania kumiliki kampuni. Ukinunua hisa, unashiriki kikamilifu kumiliki kampuni na pia unaboresha uchumi wako binafsi. Ninawasihi Watanzania wote tumieni fursa hii kununua hisa hizo kabla muda haujaisha,” alisisitiza.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema uwekezaji kwenye hisa ni njia mojawapo ya kuwawezesha Watanzania kumiliki uchumi wa nchi.
“Huko mtaani ukisema uchumi wa nchi unakua, watu wanabisha wakidai kuwa hawaoni unakua kwa sababu hawana fedha mifukoni. Hii ni fursa nyingine ya kuwawezesha kukua kiuchumi, ninaomba waichangamkie,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana, Nassama Masinda alisema amefurahishwa kuona Waziri Mkuu akinunua hisa za kampuni ya Vodacom katika soko la awali.
Mtendaji Mkuu wa Vodacom, Ian Ferrao alisema mauzo ya hisa yanayofanywa na kampuni hiyo ni makubwa mara nne ya mauzo ambayo yamewahi kufanyika hapa nchini.
Alisema kampuni hiyo ambayo imekwishafanya kazi kwa miaka 17 hapa nchini, imewekeza zaidi ya Sh2 trilioni mbili katika mtandao wa mawasiliano nchini Tanzania.
chanzo:Mwananchi.
Comments