Wataka miongozo ujenzi wa shule za ghorofa.

Kaimu Katibu mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa Shaka Hamdu ShakaWIZARA ya Elimu na Utamaduni imetakiwa kuweka miongozo ya Ujenzi wa majengo ya shule kwa ghorofa kutokana na uhaba wa maeneo ambayo mengi yamekuwa maeneo ya makazi ya watu.

Hayo yalisemwa Bagamoyo na Kaimu Katibu mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa Shaka Hamdu Shaka wakati wa ziara yake kufuatilia uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani wilayani humo na mkoa wa Pwani.


Shaka alisema kuwa kumekuwa na uhaba wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa taasisi za elimu hasa mashule ambapo miaka ijayo hakutakuwa na maeneo kabisa kwa ajili ya ujenzi hali ambayo itasababisha ujenzi huo kuwa mgumu.

“Tuzungumza na Waziri wa Elimu ili aweze kutoa mwongozo wa ujenzi wa aina hiyo kwa ajili ya maeneo ya shule ambapo kuna idadi kubwa ya watoto ambao watakuwa wakihitaji kupata elimu ambapo kwa sasa imeonekana kuna uhaba wa maeneo ya ujenzi wa shule hasa za msingi,” alisema Shaka.

Alisema kuwa kwa sasa kumekuwa na mwamko mkubwa wa wananchi kuwapeleka watoto wao shule hali ambayo imesababisha kuhitajika ujenzi wa majengo mengi ya taasisi za elimu.

Kaimu Katibu mkuu akiwa ziarani Bagamoyo alitembelea mradi wa maendeleo wa ujenzi wa nyumba ya watumishi kwenye zahanati ya Kaole pamoja na ujenzi wa madarasa na choo kwenye shule ya Msingi Muungano na jana alitarajiwa kutembelea Jimbo la Chalinze
chanzo:Habarileo.

Comments