
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein alitoa pongezi hizo Ikulu mjini Zanzibar mbele ya viongozi wa
Serikali, waandishi wa habari na Wafanyabiashara walioongozwa na
Mohammed Raza ambaye pia, ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Ahmada Yahya
Abdulwakil ambaye pia, ni Mwakilishi wa Kuteuliwa na Rais pamoja na
mfanyabiashara maarufu Said Nassor Popar.
Dk. Shein aliwapongeza wafanyabiashara hao ambao pia, baadhi yao ni
viongozi kwa mwanzo mzuri walioanza kuuonesha kwa kufanya kitendo hicho
ambacho ni faraja kubwa kwa wananchi waliopata maafa pamoja na kutoa
ushirikiano mwema na Serikali yao.
Pia, Dk. Shein hakuchelea kutumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa vyombo
vya habari kwa kutoa taarifa ya maafa hayo sambamba na wito alioutoa
kwa wale wote wenye uwezo kuwasaidia wale waliokuwa hawana uwezo ambao
wamekumbwa na maafa hayo.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa mvua hizo zimeweza kuleta athari kubwa
hasa katika kisiwa cha Pemba na kueleza kile alichokiona katika ziara
yake hivi karibuni kisiwani humo ambapo kabla ya hapo alifanya ziara
kama hiyo katika maeneo ya Unguja hasa katika Mkoa wa Mjini Magharibi
ambao ulikumbwa na mafuriko yaliotokana na mvua pamoja na upepo mkali.
Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na juhudi zilizochukuliwa na
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi , Mawasiliano na Usafirishaji kwa
hivi sasa hakuna barabara wala daraja lisilopitika katika yale
yalioharibika na mvua hizo za masika katika barabara za Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa matokeo hayo yote ni shani ya Mwenyezi Mungu hivyo
wananchi wanatakiwa wawe na subira na uvuvilivu huku akiahidi kuwa
Serikali itaendelea na juhudi za kuhakikisha wananachi wanapatiwa
misaada na maeneo yalioathirika na mvua yanafanyiwa utaratibu maalum ili
yasijekuleta madhara katika mvua zijazo.
Dk. Shein alieleza kuwa Serikali itaendelea kupokea misaada mengine
itakayotolewa huku akitoa nasaha zake kwa wafanya biashara hasa katika
kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuacha kupandisha bei za bidhaa hasa
vyakula kwani Serikali imeamua kwa makusudi kusamehe sehemu ya ushuru
wa bidhaa za vyakula ili wafanyabiashara wawauzie wananchi bidhaa hizo
kwa urahisi lakini kinachotokea ni tofauti.
Hivyo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwataka baadhi ya
wafanyabiashara kuacha mtindo huo mara moya na kusisitiza kuwa iwapo
wataendele nao serikali haitowavumilia na kusisitiza kuwa Serikali
ikiona hilo linaendelea itaurejesha ushuru huo wa bidhaa za vyakuwa
wakati wa mwezi wa Ramadhani kwani wananchi wamekuwa hawafaidiki na
chochote.
Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa matarajio yake makubwa kuwa
hapatakuwa na ubabaishaji wala hadaa katika ugawaji wa misaada hiyo
inayotolewa na wafanyabiashara na ile itakayotolewa na Serikali kwani
Kamisheni inayosimamia misdaa hiyo ina wajumbe weledi.
Katika kupambana na athari na maafa ya mvua aliahidi kuwa kwa upande
wa Bwawa la Mwanakwerekwe ambapo maji hutuama, kupitia Mradi wa Huduma
za Jamii Mijini (ZUSP) Awamu ya Pili, maji hayo yataondoshwa kwa
kuelekwezwa pwani pamoja na kujenga daraja la kisasa katika eneo la
Kibondemzungu.
Alisema kuwa Serikali inafanya tathmini juu ya athari zote
zilizotokea katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba pamoja na
athari ya upepo mkali uliotokea katika maeneo ya Mkoa wa Mjini Magharibi
huku akisisitiza akuwa Serikali ni lazima itafute jitihada za kujihami
na kukushanya uwezo kwa ajili ya maafa.
Dk. Shein alisisitiza kuwa ni vyema Serikali ikaangalia pale
inapojenga barabara ni busara ikajengwa na mitaro ya kupitishia maji
kwani athari kubwa iliyotokea katika miundombinu ya barabara nyingi hapa
nchini imetokana na barabara kukosa mitaro.
Akitoa nasaha zake kwa niaba ya wafanyabiashara hao Mohammed Raza
alieleza kuwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya Zanzibar wataendelea
kuwasaidia ndugu zao waliokumbwa na mafuriko na athari za upepo ambapo
misaada hiyo ikiwemo ya vyakula, fedha taslim na vifaa vya ujenzi
itasaidia hasa katika kipindi cha Mwezi wa Ramadhani unaokaribia.
Raza alisema kuwa kitendo hicho walichokifanya ni utamaduni wa
Wazanzibari wa kusaidiana wakati wa furaha na shida ambapo kwa upande
wake ametoa fuso nne za vyakula vikiwemo sukari pakiti 500, unga wa
ngano pakiti 500, mafuta ya kupikia katuni 100.
Nae Ahmada Yahya Abdulwakil alimkabidhi Rais TZS milioni 10 kwa
Unguja na Pemba pamoja na kuahidi msaada wa nondo tani mbili za milimita
10 zenye thamani ya TZS milioni 3 ambapo kwa upande wa mfanyabiashara
Said Nassor Popar ametoa idadi kama hiyo ya vyakula kupeleka kisiwani
Pemba ambako vitagawiwa kupitia Ofisi husika, pamoja na tende na sabuni.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk.
chanzo: zanzibar24.
chanzo: zanzibar24.
Comments