Vitabu ‘feki’ shuleni vyaichefua serikali.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo wa Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema watendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) waliosababisha kuchapisha vitabu vipya vya kiada ambavyo vina makosa wataadhibiwa.

Vitabu vya kiada vilivyobainika kuwa na makosa mengi ya usanifu, picha za vitabu kucheza na makosa ya lugha, ni vya darasa la kwanza hadi la tatu, lakini pia vimo vya sekondari. Alitoa msimamo huo wa Serikali jana wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake mjini hapa.


Alisema, pamoja na wabunge kufurahia kusambazwa kwa vitabu vya kiada vingi nchini, lakini anasikitika kwamba vitabu hivyo vina makosa mengi katika uchapaji wake. Aliongeza kuwa, kutokana na vitabu hivyo kuwa na makosa hayo, waliochangia kuchapisha vitabu hivyo, lazima watawajibika kutokana na makosa hayo.

Alisema kwa watendaji wa TET ambao wanajiona hawana sifa ya kufanya kazi hiyo hawana viwango katika kuandaa vitabu vyenye ubora, ni bora wapishe na waiache taasisi hiyo. “Wale wote waliohusika na uchapishaji vitabu ambavyo havina ubora watatakiwa kupewa adhabu kutokana na makosa waliosababisha katika kuchapa vitabu hivyo,” alisema Prof Ndalichako.

Ndalichako alikiri kwamba vitabu hivyo vina makosa na serikali imechukua hatua kuvirudisha na kuvirekebisha ili viwe katika ubora wa kutumika katika kufundishia nchini. Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Suzan Lyimo alisema, vitabu vipya vya kiada vya TET havina ubora na vina upungufu mwingi.

“Vitabu hivyo vina upungufu mkubwa ambao usiporekebishwa unaweza kusababisha madhara makubwa katika utoaji wa elimu na hivyo kushusha ubora wa elimu yetu,” alisema. Lyimo alisema serikali inatakiwa kuviondoa vitabu hivyo visitumike kwa ajili ya wanafunzi shuleni, kutokana na ukweli kwamba vina makosa mengi.

Alisema, vitabu vya kiada vya shule ya msingi hasa darasa la kwanza hadi la tatu na sekondari, vina makosa mengi ya usanifu, picha za vitabu zimecheza na makosa ya lugha, kwa hiyo havina msaada katika kuelimisha watoto.

Lyimo alisema vitabu vyote hivyo katika orodha havina viongozi wa walimu, kukosekana kwa mwongozo huo, kunachangia walimu kutopatiwa maelekezo na ufafanuzi au njia za kufundishia. Alisema kutokana na vitabu vingi kuwa na makosa serikali inatakiwa kuviondoa visitumike, japo serikali imetumika fedha nyingi kuvichapicha.

Vitabu hivyo vilianza kutumika mwaka jana na mwaka huu. Msemaji wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Bashe alisema, serikali inatakiwa kuboresha elimu ikiwa na pamoja kuhakikisha vitabu vinavyoandaliwa kwa ajili ya wanafunzi vinakuwa katika ubora ambao utasaidia kuboresha elimu nchini.

“Kamati inaishauri serikali kupitia wizara ya elimu ambayo ni mwenye dhamana wa elimu nchini kuangalia upya mfumo wa elimu na kufanya mapitio mazima na kuja na matokeo ambayo yataboreha elimu nchini kama taifa linalotaka kuwa na uchumi wa viwanda,” alisema.
Alisema vitabu ambavyo vimechapishwa kwa lengo la kupunguza pengo la vitabu vya kiada nchini, vimekuwa na makosa mengi yakiwamo ya uchapishaji, usahihi wa lugha na havina kiongozi cha mwalimu.

Katika bajeti hiyo, Waziri wa Elimu aliomba bunge liidhinishe sh trilioni 1.337 ambazo ni pungufu kwa asilimia 4.2 ya fedha ambazo ziliombwa na kuidhinishwa katika bajeti ya mwaka 2016/17 ya sh trilioni 1.396.

Kamati iliomba kwamba serikali inatakiwa kuongeza bajeti ya wizara hiyo ili angalau ifikie asilimia 10 ya bajeti kuu ya serikali ambayo ni sh trilioni 31.699. Wakichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Songwe, Philip Mulugo (CCM) alisema kitendo cha wizara kuchapisha vitabu vyenye makosa, linaitia doa serikali, inatakiwa kuangaliwa upya na watalaamu waliopo katika Taasisi ya Elimu wanatakiwa kuangaliwa upya.

Mulugo aliyewahi kuwa naibu waziri katika wizara hiyo, alisema anapenda elimu iwe bora, lakini kutokana na kuchapisha vitabu ambavyo vimekosewa kunatia doa katika elimu ya Tanzania.

Mbunge wa Vunjo, James Mbatia alisema, Serikali lazima ichukue hatua dhidi ya watu wanaotaka kuangusha elimu nchini, kwani bila kuwa na vitabu bora ni vigumu kufikia malengo ya kuondoa ujinga nchini. Elimu nchini Pamoja na matatizo hayo ya vitabu vilivyochapishwa Profesa Ndalichako alisema Serikali imefanya vizuri katika kuboresha miundombinu ya taasisi za elimu, shule za sekondari pamoja na ujenzi na ukarabati miundombinu ya shule na vyuo mbalimbali nchini.

Pia imefanya vizuri katika ujenzi wa mabweni katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) ambayo watatumia wanafunzi 3,840 na kupunguza kama si kuondoa kabisa tatizo la uhaba wa mabweni kwa wanafunzi wa chuo hicho.

"Lakini pia imefanya vizuri katika ujenzi wa maktaba ya kisasa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam ambao unaendelea na utagharimu shilingi bilioni 86.1 fedha hizo zinatolewa na Serikali ya China," alisema.

Aidha alisema Serikali imefanya vizuri pia katika kuongeza kiwango cha mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambapo bodi ya mikopo ilitoa kwa wanafunzi 122,374 ambapo wanafunzi 28,785 ni wapya na wanafunzi 93,559 ni wanaendelea na masomo. Katika kipindi kifupi serikali imefanya mambo mengi mazuri katika kuhakikisha elimu inaboreshwa nchini.
chanzo:habarileo.

Comments