Ulishawahi kujiuliza ni sekta gani inalipa zaidi ukiwa mfanyakazi ili ujaribu bahati yako? Kama bado, usipate shida.
Ripoti ya utafiti wa ajira na kipato ya mwaka 2015 (EES 2015) iliyochapishwa mtandaoni hivi karibuni na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) inabainisha kuwa sekta ya huduma za kibenki na bima ndiyo inayolipa zaidi nchini baada ya kundi kubwa la wafanyakazi wake kulipwa mshahara wa zaidi ya Sh1.5 milioni kwa mwezi.
Utafiti huo unaeleza kuwa kwa kila wafanyakazi watatu wa huduma za benki na bima mmoja anapata mshahara huo, kiwango ambacho ni kikubwa mara tano ya kima cha chini cha mshahara kilichowekwa na Serikali cha Sh310, 000.
Benki na bima inafuatiwa kwa mbali na sekta ya madini ambayo asilimia 5.9 ya wanyakazi wake wanapata mshahara wa kiwango hicho ikiwa na maana kuwa watu sita kwa kila 100 wanauhakika wa kupata zaidi ya Sh1.5 milioni kwa mwezi. Sekta nyingine zinazofuatia kwa kiwango hicho cha mshahara ni shughuli za utawala wa umma, ulinzi na hifadhi za jamii kwa asilimia 5.2 na afya na ustawi wa jamii kwa asilimia 4.4.
Uchambuzi zaidi wa takwimu hizo uliofanywa na Mwananchi unaonyesha hata kama sekta benki na bima itapimwa kwa mshahara zaidi ya Sh900, 000 kwa mwezi bado inazidi zote kwani nusu ya wafanyakazi wanaopata kiwango hicho.
Hata wakati kukiwa na sekta zinazoonekana kulipa zaidi, ripoti hiyo inaonyesha kuwa tasnia ya huduma za malazi na chakula inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanaolipwa mshahara kiduchu usiozidi Sh100, 000 kwa mwezi ambao ni asilimia 29.4.
Utafiti huo, uliofanywa kati ya Julai na Desemba 2015, unaonyesha wafanyakazi sita kati 10 wa sekta hiyo wanalipwa mshahara usiozidi Sh150, 000 wakifuatiwa na huduma za usaidizi ofisini na sekta ya kilimo, misitu na uvuvi.
Wataalamu wa masuala ya rasilimali watu wanasema kiwango cha mishahara katika sekta husika huwekwa kwa kuangalia vigezo mbalimbali vikiwemo aina ya elimu na ujuzi unaohitajika.
Mtaalamu nguli wa masuala ya rasilimali watu, Zuhura Muro alilieleza gazeti hili kwa kuwa kiwango na tija katika uzalishaji, kiwango cha ujuzi na elimu na ushindani uliopo katika sekta husika huchangia kwa kiasi kikubwa kubaini viwango vya mishahara.
“Mtu mwenye elimu ya chini katika sekta ya benki na bima ni ngazi ya cheti kwa kuwa ina vihatarishi vingi na inadhibitiwa sana ndani na kimataifa. Huwezi kuajiri mtu yeyote tu katika sekta hiyo ndiyo maana mishahara ni mikubwa,” alisema Muro ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya masuala ya rasilimali watu ya Kazi Services Limited.
Comments