Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu alibainisha hayo juzi wakati akijibu hoja za wabunge wakati wa
kupitisha bajeti ya wizara yake ya Sh 1,115,608,772,090 kwa mwaka wa
fedha 2017/2018.
Alisema atakwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali hivi karibuni kwa
ajili ya marekebisho hayo ili umri wa kuolewa ubadilishwe uwe miaka 18
badala ya miaka 14 lakini atashawishi kwa sababu maalumu mtoto aruhusiwe
kuolewa chini ya miaka hiyo 18.
“Nchini Bangladesh, nchi ya kiislamu hivi Januari mwaka huu
imerekebisha sheria yao ya ndoa na kuwa umri wa kuolewa miaka 18 lakini
kwa sababu maalumu kama mimba, mtoto anaweza kuolewa chini ya umri huo,
nami hivi karibuni nitakutana na Mwanasheria Mkuu na nitawashawishi
wenzangu tufuate hivyo kama Bangladeshi,”alisema.
Waziri huyo ameziagiza halmashauri zote nchini kupeleka maoteo ya
dawa ifikapo Januari 30 ya kila mwaka ili kuiwezesha Bohari ya Dawa(MSD)
kufikisha dawa mapema kwenye halmashauri zao tofauti na sasa
halmashauri hizo zinachelewesha maoteo hayo.
“Nataka nipimwe kwa upatikanaji wa dawa, aina 135 za dawa
zitapatikana kwa asilimia 95 mwaka huu…madaktari andikeni dawa zilizopo
hospitalini kwa wagonjwa na si zilizopo kwenye maduka yenu ya dawa na
hili tutalisimamia,”alisema.
Kuhusu huduma kwa watoto alisema wizara yake imetoa mchoro mpya wa
hospitali ambapo sasa ni lazima kila hospitali ya mkoa nchini iwe na
chumba cha kulaza watoto na hakuna ramani itakayopitishwa isiyokuwa na
chumba hicho cha kulaza watoto.
chanzo:habarileo.
Comments