Meneja wa Tanroads wa Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama,
alisema notisi ya kubomoa majengo na ukuta katika barabara hiyo
imetolewa kwa wahusika Mei 2, mwaka huu.
Alisema hakuna mwananchi yeyote aliyejenga kwenye hifadhi ya barabara
atakayelipwa fidia na kuwataka kubomoa na kupisha ujenzi huo ndani ya
siku 30 na wasipofanya hivyo taratibu za kisheria zitafuata.
“Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kumbomolea mhusika na
atalazimika kulipa gharama zote zitakazojitokeza katika utekelezaji wa
zoezi hilo. Nyumba na mali zinazotakiwa kuondolewa zimewekewa alama X”
alisema.
Mkuu wa Idara ya Mipango wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Humphrey
Kanyenye alisema ubomoaji huo umelenga upanuzi wa barabara hiyo na
miradi mingine ukiwemo wa njia sita, barabara za mwendo wa haraka na
sehemu za maegesho ya magari.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi ambao nyumba zao
zimewekwa ‘X’ wameiomba Serikali kuzungumza nao kwanza na kuwapa
utaratibu kuhusu fidia ili waendelee na ubomoaji.
Juma Abdul mkazi wa Kimara alisema wamesikia tetesi kwamba ukibomoa
haulipwi kwa madai kwamba wapo eneo la barabara lakini wanashangazwa na
hatua hiyo kwa kuwa wakati wanajenga serikali ilikuwa inaona na
haikuchukua hatua.
Neema Joseph, mfanyabiashara wa Kimara alisema Serikali inapaswa
kuangalia jinsi ya kuwasaidia wananchi hao. Naye Sikujua Athuman alisema
yeye ni mzee aliyekaa eneo hilo kwa muda, lakini anashangaa kwa sasa
kutakiwa kuvunja. Kwa upande wake, Joseph Mushi alisema kitendo cha
kubomoa nyumba kimtarudisha kijijini kwa lazima.
chanzo:Habarileo.
Comments