Serikali yasema imefanikiwa kudhibiti wizi wa mitihani.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo wa Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.SERIKALI imesema imedhibiti wizi wa mitihani kwa shule za sekondari nchini, Bunge limeelezwa. Sambamba na hilo, serikali imesema hivi karibuni itakamilisha malipo ya madeni ya walimu waliosimamia mitihani mwaka 2015 ambao hawajalipwa. Deni hilo hilo ni Sh bilioni 3.4.

Pamoja na kudhibiti wizi huo, Waziri wa Elimu , Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema kwa sasa kuna udanganyifu wa mitihani unaofanywa na walimu pindi mitihani inapofika kwenye vituo vyao wanaichomoa na kuifanya kisha majibu kuwapa wanafunzi.


“Serikali bado tunajitahidi kufuatilia kwa karibu ili kudhibiti hali hiyo, hivyo mfahamu wizi tumesha udhibiti wa mitihani isipokuwa huo udanganyifu unaofanywa na walimu,”alisema.

Akizungumzia madeni ya walimu waliosimamia mitihani mwaka 2015 ambao hajalipwa, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jafo alisema deni hilo lilikuwa Sh bilioni 6.4, serikali imeshalipwa Sh bilioni tatuna sasa deni limebaki Sh bilioni 3.4.

“Ni kweli walimu wanatudai na sasa deni lililobaki tushapeleka Hazina wanalishughulikia na lipo hatua za mwisho hivyo karibuni Sh bilioni 3.4 zitalipwa,” alisema. Jafo alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bukombe Doto Biteko (CCM) aliyeuliza lini serikali itawalipa walimu waliosimamia mitihani mwaka 2015 ambao bado hawajalipwa hadi sasa.

Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba (CCM) aliyeuliza kama serikali haioni umuhimu wa kumpima mwanafunzi kwa kutathmini tangu shule ya msingi na kuoanisha mtihani wake wa mwisho ilikupata uhalisia, Jafo alisema mfumo wa tathmini unaotumika kwa sasa unajumuisha alama za upimaji wa mwanafunzi awapo shuleni na mtihani wake wa mwisho.

“Mfano katika matokeo ya mtihani wa mwisho wa kitado cha nne, sita na ualimu kwa cheti na Stashahada , alama za upimaji wa mwanafunzi awapo shuleni zinachangia asilimia 30 na mtihani wa mwisho unachangia asilimia70,”alisema.

Alisema serikali itaendelea kufanya utafiti kwenye mifumo ya utahini inayotumika katika nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kuboresha mfumowa utahini kwa kadri itakavyoonekana inafaa na kwa kuzingatia mazingira ya utoaji wa elimu bora nchini
chanzo:habarileo.

Comments