Samia aziagiza halmashauri kujenga nyumba za wahudumu wa afya.



Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Makamu wa Rais, Samia Suluhu ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinajenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa afya hasa maeneo ya vijijini na kipaumbele kitolewe kwa wakunga ambao mara nyingi ndio wanaotoa huduma za dharura kwa wanawake wajawazito na watoto.
Suluhu ametoa agizo hilo mjini Dodoma leo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani sherehe ambazo zimehudhuriwa na mamia ya wakunga kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Amesema kuwa halmashauri zikijenga nyumba karibu na vituo vya kutolewa huduma za afya zitasaidia kupunguza matatizo ya mama na watoto wanaotaka kupata huduma za dharura ikilinganishwa na hali ilivyo sasa.
Alisema baadhi ya watumishi wa afya hasa wakunga wanakaa mbali na maeneo yao ya kazi hivyo utoaji wa huduma za dharura unakuwa duni.
Kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini, amewahakikishia wakunga na watumishi wengine wa sekta ya afya nchini kuwa Serikali inaendelea kufanyia kazi ikiwamo uboreshaji wa maslahi kwa watumishi wa kada hiyo.
chanzo:Mwananchi.

Comments