Samia ataka kasi kupunguza vifo vya uzazi.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Hassan SuluhuMAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan (pichani) ametaka kuchukuliwa hatua za makusudi ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi ambavyo vimekuwa vikiongezeka badala ya kupungua.

Aliagiza pia halmashauri zote nchini zihakikishe zinajenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa afya hasa maeneo ya vijijini na kipaumbele kitolewe kwa wakunga ambao mara nyingi ndio wanatoa huduma za dharura kwa wanawake wajawazito na watoto.


Samia alitoa maagizo hayo mjini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani, sherehe ambazo zimehudhuriwa na mamia ya wakunga kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Makamu wa Rais alisema kuwa halmashauri zikijenga nyumba karibu na vituo vya kutolewa huduma za afya zitasaidia kupunguza matatizo ya mama na watoto wanaotaka kupata huduma za dharura, ikilinganishwa na hali ilivyo sasa ambapo baadhi ya watumishi wa afya hasa wakunga wanakaa mbali na maeneo yao ya kazi hivyo utoaji wa huduma za dharura kuwa duni.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuona Tanzania inarudi nyuma wakati ilishapiga hatua katika jitihada za kutimiza lengo namba nne na lengo namba tano la malengo ya milennia na kwamba hairidhishi kuona kuwa wakati dunia imeshaanza utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030, Tanzania inaendelea kupoteza kinamama na watoto wengi.

Makamu wa Rais alisema bado Tanzania inapoteza kinamama 556 kutokana na uzazi kwa kila vizazi hai 100,000 ukilinganisha na wanawake 432 kati ya vizazi hai 100,000 miaka ya nyuma.

“Jambo hili halikubaliki ni lazima sote tushirikiane kuhakikisha kuzaa haiwi adhabu kwa wanawake,” alisema Makamu wa Rais. Pia aliwataka wakunga kuacha kauli chafu kwa mama mjamzito na kuongeza kuwa kesi za wakunga zipelekwe kwenye mabaraza yao na kama ni kosa la jinai akakumbane na sheria mahakamani.

Makamu wa Rais alisema mchango wa wakunga katika kutoa huduma za afya ya uzazi ni mkubwa na wana jukumu kubwa la kuhakikisha lengo la kuongeza kiwango cha kutumia uzazi wa mpango kinapanda kutoka asilimia 32 ya mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 45 mwaka 2020.

Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania, Feddy Mwanga alitaka wakunga wapatiwe makazi karibu na vituo vya afya kwani itasaidia huduma kuwepo kwa saa 24. Kaulimbinu ya maadhimisho ya Siku ya Wakunga mwaka huu ni “Wakunga, Akinamama na Familia ni washirika wa Kudumu.”
chanzo:Habarileo.

Comments