Profesa Rwekaza Mkandala ambae ni
Makamu Mkuu wa UDSM, alisema idara ambazo watumishi wake walibainika
wakutumia vyeti feki ni polisi, madereva, mapokezi, na watumishi wa kada
ya chini.
“Kazi ya uhakiki mbona
ilishakamilika muda mrefu? Watumishi 24 walibainika wana vyeti feki na
wengine 128 vyeti vyao vina utata, na idara zilizobainika ni hizi ndogo
ndogo,” alisema Profesa Mkandala.
Alipoulizwa ni kwa namna gani watumishi 128
vyeti vyao vina utata, Prof. Mkandala alisema baadhi havionekani katika
mfumo wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta).
Alisema UDSM bado inaendelea kuvifanyia uchunguzi vyeti hivyo na iwapo itabainika kuwa ni vya kughushi nao watafukuzwa kazi.
Kazi ya uhakiki wa vyeti vya elimu na taaluma
kwa watumishi wote wa umma ilianza Machi mwaka jana lengo kuu likiwa ni
kuongeza ufanisi katika kazi ya kuwatumikia Watanzania pamoja na kutoa
nafasi za ajira kwa Watanzania wenye sifa kitaaluma.
Tangu kuanza kwa ukaguzi huo, zaidi ya
watumishi 9,932 walibainika wakitumia vyeti bandia wakiwamo waliokuwa
wakihudumia taasisi nyeti kama Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambayo
watumishi wake 134 walikutwa na vyeti feki.
Baada ya kupokea taarifa ya ukaguzi iliyobaini
watumishi hao karibu 10,000 mwezi uliopita, Rais Magufuli alimwagiza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela
Kairuki, kuwatangazia waondoke mara moja katika nafasi zao za kazi kabla
ya Mei 15, vinginevyo wangechukuliwa hatua kali za kisheria, sambamba
na kutangaza nafasi mpya za ajira.
Hadi sasa inaelezwa kuwa ofisi mbalimbali za
Serikali zimekuwa na upungufu wa watumishi baada ya wafanyakazi hao
kubainika wakitumia vyeti bandia.
chanzo: zanzibar24.
Comments