
Gazeti hili lilishuhudia umati huo wa watumishi ukiwa umekusanyika
katika ofisi hizo za Necta zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam huku
baadhi yao waliowahi wakipewa namba na kuingia ndani kuwasilisha vyeti
na wengine wakisubiri nje kupangiwa utaratibu.
Akizungumza na gazeti la Habari leo jana, Ofisa Habari wa baraza
hilo, John Nchimbi alikiri baraza hilo kupokea umati mkubwa wa watumishi
hao wanaokata rufaa ambao wanaongezeka kila siku.
Nchimbi alisema kwa sasa kuna makundi matatu ya watumishi hao
yakiwemo kundi la watumishi walioghushi vyeti, watumishi waliowasilisha
vyeti visivyokamilika na watumishi wenye vyeti vyenye utata ambavyo
cheti kimoja kinatumiwa na zaidi ya mtumishi mmoja.
“Kiutaratibu sisi Necta tunatakiwa kuwashughulikia watumishi waliopo
kwenye orodha ya vyeti vyenye utata, tunamtaka mtumishi aliyekata rufaa
awasilishe vyeti vyake halali kwetu tunampa namba na anaondoka zake,”
alisema Nchimbi.
Hata hivyo, alifafanua kuwa pamoja na ukweli huo, makundi yote matatu
yamejitokeza na kuwasilisha rufaa na malalamiko yao Necta jambo ambalo
baraza hilo inabidi liwahudumie.
Alisema kiutaratibu watumishi ambao vyeti vyao havijakamilika,
wanatakiwa kuwasilisha rufaa zao kwa waajiri wao na vielelezo baada ya
hapo waajiri hao watawasilisha mbele ya baraza hilo rufaa hiyo
iliyoambatana na vielelezo.
Kwa upande wa watumishi wenye vyeti vya kughushi wanapaswa
kuwasilisha rufaa zao kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala wa Bora ambaye ndiye atakayewasilisha rufaa
hizo kwa baraza hilo la mitihani.
“Bahati mbaya kwa sasa wote wanakuja kwetu lakini tunawahudumia,
tunajitahidi kuhakikisha kila mtu anapata haki yake, utaratibu mzijma
ukikamilika kwa tarehe iliyotangazwa na Rais John Magufuli, tutapeleka
idadi ya waliokata rufaa na matokeo kunakohusika,” alifafanua.
Baadhi ya watumishi waliojitokeza katika eneo hilo la Necta,
walioomba kutotaja majina yao kwa usalama wao kikazi, walibainisha kuwa
wameamua kukata rufaa kwa kuwa wana uhakika hawajaghushi vyeti vyao.
“Mimi nimeshangaa kuliona jina langu kwenye orodha ya walioghushi
kwanza nimeshtuka sana, nimeambiwa vyeti vyangu vinatumiwa na watu
wengine ambao hata siwajui, nimekuja hapa kuthibitisha kuwa mimi ndio
mmiliki halali wa vyeti vyangu,” alisema mmoja wa watumishi hao
aliyetambulisha kuwa anafanya kazi kwenye halmashauri.
Chanzo: Habari leo
Comments