
Aidha Sadiki alisema pia kulingana na afya yake, anahitaji kupisha
vijana wadogo wamsaidie Rais Dk. John Pombe Magufuli kulingana na kasi
yake kwani yeye ameepuka kumkwaza rais wakati wa utekelezaji wa majukumu
yake kama mkuu wa mkoa. “Uamuzi huu wa kupumzika nilimuomba rais kwa
muda mrefu sana, na nikirudi kijijini nitaendelea na ufugaji Samaki
maana nilishaandaa bwawa la kufugia, nitaendelea nalo huku nikiwaza
jambo lingine la kufanya,” alisema.
Sadiki alisema hayo jana wakati wa mahojiano maalum na gazeti la
Habarileo kuhusu sababu zilizochangia kumuomba Rais Magufuli kuacha kazi
yake ya ukuu wa mkoa wa Kilimanjaro.
“Namshukuru rais kuridhia ombi
langu, nimetumikia serikali tangu mwaka 1999 nikiwa mkuu wa wilaya na
baadaye mkuu wa mkoa kuanzia mwaka 2005 hadi sasa ninapoondoka mwenyewe…
nimeona ni wakati muafaka kumweleza aliyeniteua kuwa nahitaji kupumzika
nikiwa na akili timamu na afya njema,” alisema.
Alisema Sababu nyingine kubwa ni kuhofia afya yake kutomudu kasi ya
rais Magufuli, kwani alifanyiwa upasuaji mwaka 2012 na 2014 nchini India
ingawa hakutaka kuweka wazi maradhi yaliyokuwa yakimkabili. “Kama
kiongozi muungwana lazma ifike mahali ukiri kwamba wapo vijana wenye
uwezo mzuri na kasi ambayo inaendana na serikali ya awamu ya tano… mimi
nilishatekeleza wajibu wangu na mchango kwa serikali yangu, sasa
inatosha, tupate mawazo na michango ya wengine,” alisema.
Sadiki ambaye amekuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro tangu Machi 13,2016
alipoteuliwa na Rais Magufuli, alisema siyo vibaya kwa kiongozi
kujitathmini na kuwaachia wengine kama atabaini kasi yake ya utendaji
kazi imeanza kupungua. Kwa upande wake Afisa Habari wa mkoa huo, Shabani
Pazi alisema mkoa umeshtushwa na uamuzi wa mkuu wa mkoa kwani hawakuwa
wameuratajia kwani tangu amefika mkoani humo watumishi walioko chini
yake walianza kumuelewa na kwenda na kasi yake.
“Ni jambo la mshtuko maana sisi kama watumishi wa ngazi za chini,
kiongozi anapoteuliwa mnajifunza yale mema anayotenda na kujaribu
kufauata kasi yake… sasa tumeanza kumuelewa nini vipaumbele vyake,
anahitaji nini, tunashangaa yaliyotokea,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, mkuu wa mkoa Sadiki pamoja na aliyekuwa jaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebeisha
Sheria Tanzania, Aloysius Mujulizi na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Upendo Msuya waliomba kuacha kazi na rais akaridhia
Chanzo: Habari Leo
Comments