Inakadiriwa kuwa Nyumba zipatazo 77 zimeezuka mapaa na nyengine
kufanya ufa kufuatia Upepo mkali uliovuma mapema leo asubuhi katika
maeneo ya Mitaa ya Pangawe, Nyarugusu, Mwanakwerekwe na Kinuni ndani ya
Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa wa Mjini Magharibi.
Upepo huo umesababisha Watu Wawili kujeruhiwa katika maafa hayo
ambapo Mmoja alikatwa na Bati wakati mwengine alijeruhiwa kwa kuangukiwa
na Tofali wakati wa kizaa zaa hicho cha ghafla.
Mashuhuda wa tukio hilo waliviambia vyombo vya Habari kuwa upepo huo
ulivuma ghafla na kutoa cheche za moto ambazo ghafla waliuona ukiezua
mapaa kukata baadhi ya majengo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika
katika eneo hilo ili kuwafariji na kuwapa pole Wananchi walioathirika na
janga hilo lililowaacha katika mazingira magumu ya makaazi.
Akitoa Taarifa za awali ya Athari ya Upepo huo Mkuu wa Mkoa Mjini
Magharibi Mheshimwa Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Serikali ya Mkoa
kupitia Wilaya ya Magharibi “B” kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa ya
Wilaya hiyo na ile ya Taifa imeanza kufanya tathmini ili kujua hasara
iliyojitokeza kutokana na janga hilo.
Mh. Ayoub alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
kwamba juhudi za Serikali ya Mkoa Mjini Magharibi katika kuwahami
Waathirika hao imejitolea kusaidia Kilo 25 za Mchele kwa kila Familia
iliyokumbwa na janga hilo.
Mkuu huyo wa Mkoa Mjini Magharibi kupitia Balozi Seif ambae pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar aliwaomba
wafadhili na Wafanyabiashara ndani na nje ya Nchi kusaidia janga hilo
kwa lengo la kuwafariji waathirika wa Upepo huo.
Akitoa mkono wa pole pamoja na kuwafariji Wananchi hao wa Mitaa ya
Pangawe na Nyarugusu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alisema amepata Taarifa ya tukio hilo akiwa katika vikao vya Baraza
la Wawakilishi na kuamua kukatisha ili kufika kuwafariji Wananchi hao.
Balozi Seif alisema hilo ni tukio lisolotegemewa kutokea ghafla kiasi
hicho jambo ambalo waahtirika hao wanapaswa kuendelea kuwa na subira
katika kipindi hichi kigumu cha maafa.
Aliwahimiza Wananchi waendelee kusaidiana kama walivyoonyesha
mshikamano wao wa kusaidia kwenye janga hilo jamii ibakie kuwa na
utulivu na kuendelea kuishi katika maisha ya kawaida.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa Wananchi wote hapa Nchini
kuwa na tahadhari na mvua zinazoendelea kunyesha kwa vile bado
zitaendelea kutokea hadi mwishoni wa mwezi huu wa mei kwa Unguja Na
Mwanzoni mwa Mwezi wa Juni kwa Kisiwa cha Pemba.
Picha zinazofuata ni maafa ya upepo Kinuni, Nyarugusu, Mwanakwerekwe na Pangawe Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa Mjini Magharibi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipofanya ziara ya
kuwafariji waathirika wa upepo katika Mitaa ya Nyarugusu, Kinuni,
Mwanakwerekwe na Pangawe Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa Mjini Magharibi
Unguja.






Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
15/5/2017.
chanzo: zanzibar24.
Comments