Mwanafunzi atoweka katika mazingira ya kutatanisha.



 Fatma Jabir
Mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari Kange
jijini hapa, Fatma Jabir (15)  ametoweka  kwa wiki mbili sasa huku
jitihada za kumpata zikishindwa kuzaa matunda.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amesema mwanafunzi huyoalitoweka nyumbani tangu Mei 6 mwaka huu na hadi sasa hajapatikana.
Mama wa mwanafunzi huyo, Swahiba Hashim (39) amesema kuwa mwanaye
aliondoka nyumbani Jumamosi na kuaga kuwa anaenda kwa rafiki yake wa kike anayeishi Kichangani.

Swahiba ambaye ni mfanyabiashara ya duka amesema aliporejea nyumbani jioni kutoka kwenye mizunguko yake mwanaye hakuwa amerudi.
"Nikaenda kituo cha polisi kutoa taarifa nikapewa saa 24 za kusubiri
ilipofika Jumatatu nikaenda tena kuwaambia kwamba hajarudi ndipo
akakamatwa rafiki yake ambaye alipofikishwa kituoni licha ya kupigwa
sana lakini alidai kwamba hajui aliko,"amesema.
Mama huyo amesema  jitihada za kumpata zimeshindikana kwa kuwa
ameshawasiliana na ndugu zake walioko mikoa mbalimbali ambao wamesema
hajafika kwao na hata shuleni hajaonekana.
"Nisadieni jamani nimuone mwanangu kwani sijui kama ameuawa au yuko
wapi nataka nimuone tu kwani hapa nilipo siwezi kula wala kufanya
chochote,"amesema Swahiba.
 chanzo:Mwananchi.

Comments