Mvua yaua 7 na kujeruhi 10, Mkoani Tanga.

IDADI ya wakazi waliokufa kutokana na athari za mvua ya masika inayoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga, imefikia saba sasa wakiwemo wanawake watano, wanaume wawili pamoja na majeruhi 10.

Vifo hivyo vyote vimetokana na maporomoko ya maji, mawe, miti na mchanga kutoka katika Milima ya Usambara Magharibi ambavyo vimeendelea kuvamia kwa kasi baadhi ya nyumba zilizo mabondeni katika kata za Mkumbara, Chekereni, Makuyuni, Kwagunda, Kerenge na Ngombezi.


Pia Imebainika kwamba hali ya usalama kwa baadhi ya wananchini mbaya  hasa wale wasiotaka kuhama kwenye nyumba zao zilizoko bondeni jirani na kingo za Mto Pangani na kusababisha  wanyama wakali akiwemo mamba kuanza kuvamia nyumba hizo ili kutafuta malisho.

Akizungumza jana jioni katika mahojiano kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel alisema hali ya uslama kwa wakazi wa maeneo hayo haijatengemaa hivyo jamii inapaswa kufanya kila linalowezekana ili kuokoa maisha.

“Kuna tukio la kusikitisha sana la jana huko Kata ya Ngombezi ambako ni jirani na mto Pangani kuna mama mmoja amenusurika kuliwa na Mamba wakati alipokuwa akisafisha kifaa cha kudekia nyumba kwa kutumia maji hayo ya mafuriko,”

Alisema mkuu wa wilaya na kuongeza: “Ilikuwa tu baada ya kumaliza usafi akaamua kwenda kusuuza dekio bila kujua kwamba kumbe mamba alikuwa mawindoni ametoka huko mtoni na kujichanganya kwenye hayo mafuriko jirani na nyumba wakati mama akiendelea kusafisha ndipo mamba akavamia hilo dekio na kuondoka nalo na mama akanusurika.”

 chanzo:zanzibar24.

Comments