Mvua yaliza wabunge.

Wakazi wa Videte Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani wakivuka mto Mzinga kwenda Bamia karibu na Uwanja wa Azam Complex Chamazi Manispaa ya Temeke Dar es Salaam. Wakazi hao wameomba kusaidiwa daraja kwa kuwa uvushaji huo ni hatari kwa maisha yao hasa kipindi hiki cha mvua. Wakazi hao wanavushwa kwa shilingi 1000 kwa kila kichwa.ATHARI za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko na maporomoko katika sehemu mbalimbali nchini jana ziliwagusa wabunge na kutaka Bunge liahirishe shughuli zake ili wabunge waijadili hali hiyo iliyoathiri miumdobinu, makazi na hata kusababisha vifo.

Mvua hizo zinazoendelea kunyesha kwa takribani wiki tatu mfululizo sasa, zimeacha athari kubwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Zanzibar. Wabunge walioomba mwongozo baada ya kumalizika Kipindi cha Maswali na Majibu ni Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), Mbunge wa Vunjo James Mbatia (NCCR Mageuzi) na wa Mlalo, Rashid Shangazi (CCM).


Ngonyani maarufu kama Profesa Majimarefu alisema kuna matatizo makubwa ya mafuriko nchini. 

“Kwenye mkoa wangu wa Tanga kumekuwa na maafa, leo (jana) hii kuna watu 1,000 hawana chakula, mahali pa kuishi na hawana msaada wowote, lakini serikali itawasaidiaje hawa watu wakati kamati za afya zikiendelea na utaratibu,”alisema. Kwa upande wa Shangazi alitaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili wabunge wajadili kuhusu mafuriko hayo.

“Sasa hivi katika mkoa wa Tanga kuna mafuriko makubwa sana. Jana (juzi) yametokea maporomoko katika milima ya Usambara, eneo la barabara za Lushoto- Arusha- Mombo , Pangani kwenda Tanga, Mombo kwenda Lushoto na Kilindi kwenda Morogoro zote zilifungwa,”alisema.

Alisema Mkoa wa Tanga umegeuka kuwa kisiwa umepata athari kubwa hasa Korogwe na kuiomba Serikali ilione hilo jambo ni la kimkakati na kwamba Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) amezidiwa .

Alisema barabara hizo zimekuwa zikiunganisha mkoa huo na mikoa mingine na kutaka Bunge lijadili angalau kwa muda mfupi. 

Naye Mbatia alisema hali ni tete kutokana na mafuriko yaliyojitokeza na kuomba utu wa mwanadamu kuzingatiwa kama wawakilishi wa Watanzania kwa kutenga muda wa angalau dakika 15 kujadili suala hilo.

“Tutenge muda wa dakika 15 ama 20 ili tujadili suala hili, ambayo ni ya maafa tunaweza tukatoa majibu sahihi kwa wapiga kura wetu, mwenyekitindio ombi langu kwa mujibu wa kanuni nilizozitumia,”alisema.

Akijibu miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alisema miongozo ya Mbatia na Shangazi imeangukia katika kanuni ya 47 (1) ambayo inasomwa pamoja na kanuni ya 48. “Lakini kanuni ya 47(4) inampa Spika mamlaka aridhike kama ombi hilo anaona jambo hilo kweli linahitaji kusitisha shughuli zilizo mbele yetu ili kujadili hoja hizo za dharura,”alisema.

Hata hivyo, alisema kwa hali anayoiona haoni kama suala hilo linahitaji kujadiliwa sasa. “Ni kweli tukio hili limegusa maeneo mengi, nawapa pole walioguswa kwa namna moja hata nyingine. 

Naamini Serikali iliyoko humu ndani itaitolea maelezo wakiangalia nchi nzima,”alisema na kuongeza kuwa, anaamini Serikali italizungumzia vizuri kuliko kila mbunge kujisemea katika eneo lake.

Kuhusu mwongozo wa Ngonyani, Chenge alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 68 (7) ni lazima liwe tukio ama jambo ambalo limetokea mapema bungeni na si nje. Polisi asombwa, afa Wakati wabunge wakitaka kujadiliwa kwa athari za mvua zinazoendelea kunyesha, askari wa Jeshi la Polisi, Abbas Anas Haji (55) amekufa maji baada ya kusombwa akiwa na pikipiki yake aina ya Vespa wakati akipita eneo la barabara ya Fuoni Kibondemzungu lililofunikwa na maji. 

Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 5:30 asubuhi wakati askari huyo akitokea kazini kwenda nyumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Hassan Nassir Ali alisema marehemu alikuwa ni mfanyakazi wa jeshi la polisi katika Kitengo cha Picha, Makao Makuu ya Polisi upande wa Zanzibar.

Familia 150 zatangatanga Katika tukio jingine, zaidi ya familia 150 kisiwani Pemba zimekosa makazi na kulazimika kusitiriwa na ndugu na jamaa baada ya nyumba zao kuathirika vibaya na mvua kubwa iliyonyesha kwa siku tatu mfululizo.

Timu ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyotembelea mikoa miwili Pemba na kujionea athari za mafuriko, imeelezea kufurahishwa na mshikamano mkubwa uliooneshwa na wananchi katika kusaidiana bila ya kujali itikadi za kisiasa.

Waziri asiye na Wizara Maalumu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Juma Khatib alisema wananchi wameonesha uzalendo wa hali ya juu ambao watu wote walioathirika na mafuriko hayo wamehifadhiwa na kuishi kwa ndugu na jamaa.

Aidha, Khatib waliwataka wananchi walioathirika na mafuriko hayo wasirudi tena katika maeneo yao hayo ambayo athari zake bado zipo. Ameahidi kusaidia na kutoa mifuko ya saruji 50 kwa familia za wilaya ya Mkoani ili zikarabati nyumba zao.

Tanga-Arusha yafunguka Aidha, mkoani Tanga ambako miundombinu ya barabara ilisababisha kukusekana kwa usafiri kati ya mkoa wa Tanga na mikoa jirani ya Kilimanjaro na Arusha, hali imetajwa kurejea katika hali yake ya kawaida.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel akizungumza jana katika mahojiano kwa njia ya simu alisema kiasi cha mvua inayonyesha kimeanza kupungua ingawa ipo hali ya mawingu mazito katika baadhi ya maeneo.

Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba akizungumzia hali ya usalama kuhusu kifusi kilichoanguka na kufunga sehemu ya eneo la barabara kuu inayounganisha miji ya Soni na Lushoto alisema anaelekea eneo la tukio na kwamba atatoa taarifa.

Aidha, kuhusu mawasiliano ya barabara ya Tanga - Pangani alisema kwa sasa watumiaji wa barabara hiyo wanapita katika njia mbili mbadala ikiwemo ya Pongwe - Kirare jijini Tanga pamoja na ile ya Muheza- Misozwe - Pangani ya wilayani Muheza wakati huu ambapo Tanroads wanafanya jitihada za kutengeneza njia ya mchepuko katika eneo la daraja la Neema lililopo kwenye barabara kuu ya Tanga- Pangani.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa ameuagiza uongozi wa Jiji la Tanga kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wajitahidi kufanya utafiti wa maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja nyakati za msimu wa mvua badala ya kiangazi ili kupata picha ya mahitaji halisi ya ujenzi tofauti na inavyofanyika sasa.

Ametoa maagizo hayo kwa nyakati tofauti jana alipozungumza katika mahojiano na HabariLeo baada ya kutembelea baadhi ya mitaa ya jijini Tanga iliyoathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua isiyo ya kawaida iliyonyesha mfululizo juzi kwa saa 24 na kusababisha maafa ikiwemo vifo vya wakazi wawili.

Katika mji wa Tanga, mvua hizo ziliua watu wawili, nyumba 97 zilizingirwa maji pamoja na Soko maarufu la vyakula la Magandini na kusababisha mali zote kupotea, nyingine 36 zilibomoka kabisa, moja kutitia, nyingine kuteketea kwa ajali ya moto uliotokana na hitilafu ya umeme ambapo kaya 59 zenye wakazi zaidi ya 200 walioathirika walihifadhiwa katika kambi zilizopo kwenye shule ya msingi ya Chumbageni, Kwakaheza, Magaoni, Mafuriko na Sekondari ya Hotten.

Mvua za kihistoria Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) hivi karibuni ilitoa taarifa inayoonesha kuwa, mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali mkoani Tanga zimefikia kiwango cha juu ambacho hakikuwahi kurekodiwa tangu mwaka 1949, sawa na takribani miaka 68 iliyopita.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Utafiti wa mamlaka hiyo, Dk Ladislauds Chang’a, mvua iliyonyesha kwa saa 24 Mei 9 mwaka huu mkoani Tanga ni ya milimita 316, kiwango ambacho hakijarekodiwa kwa miaka mingi.

Aliongeza kuwa, hawajafanya tathimini, lakini mwaka 2014 kulikuwa na kiwango kikubwa zaidi baada ya kunyesha mvua ya milimita 138 ndani ya saa 24 na kwamba kiwango cha juu kwa historia ya kituo cha Dar es Salaam ni mwaka 1953 iliponyesha mvua ya kiwango cha milimita 167.4. 

Alisema mvua za sasa zinatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi huu.

Imeandikwa na Maulid Ahmed (Dodoma), Anna Makange (Tanga) na Khatibu Suleiman (Zanzibar).
chanzo:Habrileo.

Comments