Kama ilivyo kawaida, mvua hizo hutoa fursa ya ajira ya kubeba watu kuwavusha katika madimbwi, lakini safari hii imeibua ajira mpya ya kuwanawisha miguu .
Mteja hutozwa Sh200 kwa huduma hizo katika soko hilo lililojaa matope na maji na vijana na kina mama ambao wamepanga ndoo za maji nje ya lango la soko, wakiita wateja kwa lugha ya bashasha kuwashawishi wanawishwe miguu na kubebwa.
“Karibu dada unawe miguu. Dada tukubebe? Sh200 tu. Njoo unawe miguu yako hapa maji safi kabisa yamethibitishwa na TBS,” alisema mmoja wa vijana hao akimkaribisha mwandishi wa Mwananchi eneo hilo.
Vijana hao walisema wameanza biashara hiyo baada ya mvua kusababisha maji kujaa na kusababisha tope.
“Tumeamua kujiongeza maana tumeona watu wanatoka ndani wamechafuka na kwenda kununua maji ya dukani kusafisha miguu yao. Tukaona kwa nini tusifanye biashara ya kuwaosha miguu.Tukaona ni fursa basi tukaitumia,” alisema kijana aliyejitambulisha kwa jina la Omary Mohamed.
Vijana hao walisema kwa siku wanapata kati ya Sh30,000 na Sh50,000 kulingana na wingi wa wateja wanaoingia sokoni.
“Tunatumia maji ya bomba ambayo pia tunanunua ndoo Sh200 kisha tunawaosha kwa kutumia brashi za vipande vya godoro na mifuko ya sandarusi,” alisema kijana mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Leonard Marko.
Swaumu Abeli, mmoja wa kina mama wanaotoa huduma ya kuosha miguu na kukodisha viatu vya mvua (gumboot) alisema biashara hiyo imemsaidia kuongeza kipato katika familia yake.
“Hapa sokoni mimi nafanya biashara ya kuuza maji ya kandoro. Sasa mvua hizi zilivyoanza kunyesha soko likawa limepungua, lakini nikaona kuna fursa ya biashara nyingine ya kuosha watu miguu na kukodisha gambuti. Nikaamua kufanya,” alisema Abeli.
Alisema anakodisha viatu hivyo kwa Sh1,000 na kuwaosha miguu watu kwa Sh 200 na kwa siku anaweza kupata Sh30,000.
Wakati wengine wakifurahia na kuomba mvua ziendelee, wauzaji matunda, vyakula na wamiliki wa migahawa sokoni hapo wanadai bidhaa zao zinaoza.
“Soko ni chafu, maji yanajaa tunakosa hata sehemu ya kuweka matunda. Kama unavyoona tunaweka matunda kwenye maji na yanaoza. Serikali itusaidie,” alisema Husna Juma.
Hata hivyo, baadhi ya wateja wanaokwenda sokoni hapo kununua bidhaa wamelalamika kuwashwa na maji machafu wanayokanyaga na kuhofia afya zao.
“Haya maji tunayokanyaga ni machafu tunawashwa miguu. Serikali iliangalie hili soko, hali si nzuri inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa,” alisema Jumanne John.
Mvua zilianza kunyesha nchini kote Machi na Mamlaka ya Hali ya Hewa imeshaeleza kuwa zitaendelea hadi katikati ya mwezi huu.
chanzo:Mwananchi.
Comments