Ziara ya Profesa Muhongo katika machimbo yaliyopo wilayani Sikonge,
ilifanyika Mei 8, mwaka huu, ambayo ililenga kuwafariji wananchi,
kuzungumza na wamiliki wa migodi pamoja na wachimbaji na kutoa mwongozo
wa serikali kuhusu hatua za kufuatwa ili kuhakikisha shughuli za
uchimbaji wa madini zinafanyika kwa usalama.
Akizungumza na wananchi baada ya kukagua eneo yalipotokea maafa,
Profesa Muhongo alitoa muda wa siku tatu kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi
nchini, Ally Samaje kwa kushirikiana na Ofisi ya Madini Kanda ya
Kati-Magharibi, Ofisi ya Ofisa Madini Mkazi Tabora pamoja na Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa husika ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Aggrey
Mwanri, kufanya ukaguzi na kuchukua hatua zitakazohakikisha shughuli za
uchimbaji mahala hapo zinafanyika kwa usalama.
Akifafanua zaidi kuhusu mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na timu
hiyo ya ukaguzi, alisema ni lazima ipatikane orodha kamili ya wananchi
walio tayari kufanya kazi katika migodi husika ili wajulikane, kukagua
kwa kina eneo lote la migodi ili kujionea hali halisi pamoja na kutoa
mwongozo/ushauri kwa wamiliki wa leseni husika kuhusu namna bora ya
kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini kwa njia salama.
Akizungumza hilo, Samaje, kwa niaba ya timu iliyoagizwa na waziri
kushughulikia hatua za kiusalama, alisema tayari wamekamilisha kazi
waliyopewa na kwamba wamewapatia mwongozo wa utendaji kazi wamiliki wa
leseni husika.
Alitaja baadhi ya mambo muhimu ambayo timu hiyo imeshughulikia kuwa
ni pamoja na kutoa maagizo katika eneo la mgodi wenye leseni ya
uchimbaji mdogo wa madini namba 002211 CWZ, inayomilikiwa na kikundi cha
WINIMA, na ambalo ndilo lilihusisha vifo vya watu sita kwa kufukiwa na
kifusi, kuwa na mashimo ya uchimbaji 16 tu badala ya 200 yaliyokuwepo
awali.
chanzo:Habarileo
Comments