
Msemaji wa jeshi hilo amesema mtambo huo sasa una uwezo wa
kuzuia makombora yanayorushwa na Korea Kaskazini na pia kuilinda Korea
Kusini.
Lakini maafisa wameambia wanahabari kwamba itachukua miezi kadha kabla ya mfumo huo katika kutumika kikamilifu.
Hali ya wasiwasi imekuwa ikitanga katika rasi ya Korea, huku Korea Kaskazini ikiendelea kutoa vitisho mara kwa mara.
Marekani nayo imetuma kundi la meli za kivita pamoja na nyambizi katika rasi hiyo.
Jumatatu, ndege mbili za kuangusha mabomu za Marekani zilifanya
mazoezi ya pamoja na jeshi la wanahewa la Korea Kusini, operesheni
ambayo Marekani ilisema ilikuwa ya kawaida.
Mtambo wa Thaad, ambao
kwa kirefu husimamia Terminal High Altitude Area Defence, ulianza
kuwekwa wiki iliyopita katika eneo ambalo zamani lilikuwa uwanja wa gofu
katika eneo la Seongju katikati mwa Korea Kusini.
Baadhi ya raia wa Korea Kusini waliandamana kuupinga.
Wengi wa wenyeji wanaamini mtambo huo unaweza kulengwa na adui na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wanaoishi hapo karibu.
China pia imepinga kuwepo kwa mtambo huo - ikisema uwezo wake wa rada huenda ukahitilafiana na operesheni zake za kijeshi.

Lakini afisa mmoja wa ulinzi wa Marekani aliambia shirika la habari
la AFP kuwa mfumo huo kwa sasa una uwezo tu wa "kuzuia makombora hatua
ya awali" lakini unaimarishwa baadaye mwaka huu vifaa zaidi vya mtambo
huo vitakapowasilishwa.
Korea
Kaskazini na Marekani zimekuwa zikijibizana vikali wiki za hivi
karibuni huku Pyongyang ikiendelea kupuuza marufuku ya Umoja wa Mataifa
inayoizuia kufanya majaribio ya makombora.
Taifa hilo lenye usiri
mkubwa limetekeleza majaribio mawili ya makombora, ambayo yalifeli, wiki
za karibuni, na limesema kwamba liko tayari kufanya jaribio lake la
sita la nyuklia wakati wowote.
THAAD ni nini?
- Ni teknolojia ya kujilinda ya kutungua makombora ya masafa mafupi na wastani ambayo huyaharibu yanapokaribia kulipuka.
- Hugonga kombora la kuliharibu
- Ina uwezo wa kufika umbali wa kilomita 200 na inaweza kurushwa juu hadi kilomita 150 angani
- Marekani imewahi kuweka mitambo kama hiyo Guam na Hawaii kujilinda dhidi ya uwezekano wa mashambulizi kutoka kwa Korea Kaskazini
chanzo:Bbc.
Comments