Mradi wa maji Matemange wagubikwa na harufu ya ufisadi.

Mwenge wa UhuruKIONGOZI wa Mbio za Mwenge kitaifa, Amour Hamad Amour amegoma kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wa Matemanga wilayani Tunduru kutokana na mradi husika kutokamilika na kuwepo kwa mazingira ya ufisadi.

Mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia mpaka utakapokamilika utakuwa umegharimu Sh 1,039,000,000. Taarifa ya mradi huo ambao bado kukamilika, zinasema kwamba mkandarasi Cosmos Engineering Co Ltd ambaye ndiye anayejenga mradi huo ameshalipwa tayari Sh milioni 300 za awali.


Aidha, fedha nyingine Sh milioni 200, alilipwa lakini akanasa katika tatizo la kodi ya serikali. Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge alisema wao hawawezi kuweka jiwe la msingi la mradi kutokana na halmashauri kutotoa vielelezo vya kutosha.

Kwa mujibu wa mkataba mradi ulipaswa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2013/14 na kukamilika katika kipindi cha miezi sita. 

Amour alisema Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imelea mkandarasi huo ambaye anaonekana kuwa dhaifu katika utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa maji.

Amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera kufanya uchunguzi dhidi ya utendaji kazi wa mkandarasi Cosmos Engineering, kutokana na kuonesha utendaji usioridhisha na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watumishi wa halmashauri hiyo waliohusika.

Naye Mbunge wa Tunduru Kaskazini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani amesema mradi wa maji wa Matemanga umekuwa na changamoto nyingi tangu uanze kutokana na fedha kuchelewa.

Pia alisema mkandarasi ameonekana kutokuwa na uwezo wa kifedha wa kuendesha mambo yake akisuburi malipo ya serikali. Awali, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru iliwahi kuvunja mkataba na mkandarasi Cosmos kwa kile kilichoelezwa ni kushindwa kutekeleza mradi huo mwaka 2016.

Hata hivyo, katika mazingira yanayotia shaka halmashauri hiyo Aprili 2017 ilimwongezea mkataba wa miezi miwili mkandarasi huyo na kutakiwa akamilishe mradi ifikapo Juni 2017 kitu ambacho kiongozi huyo wa mbio za Mwenge alisema hapendezwi nacho.
CHANZO:habarileo.

Comments