
Gambo aliyasema hayo katika taarifa yake kupitia vyombo vya habari
aliyoitoa jana kuwa hivi karibuni, ofisi yake ilitoa taarifa ya mapato
na matumizi kuhusu michango ya rambirambi ya ajali ya basi ya shule ya
Lucky Vincent iliyotokea Wilayani Karatu eneo la Rhotia. Alisema ajali
hiyo ilipotezea watu 35, wakiwemo wanafunzi 32, walimu 2 na dereva 1.
Aidha, ajali hiyo pia ilibakiza majeruhi 3 ambao ni Wilson Tarimo,
Sadya Awadh na Doren Elibariki na kwamba hali zao zinaendelea vizuri
huku akisema anaamini Mwenyezi Mungu ana makusudio yake kuwaacha.
RC Gambo alisema baada ya serikali na wadau mbalimbali nchini
kushirikiana kufanikisha kuihifadhi miili, ikiwa ni pamoja na kutoa
rambirambi ya Sh 3,857,000 kwa kila familia iliyofiwa. Alisema hivi sasa
wameona ni vema nguvu kubwa ikaelekezwa kwenye kuwahudumia majeruhi ili
waweze kupona na makusudio ya Mungu yaweze kutimia.
“Tunapenda kuujulisha Umma kuwa hadi Ijumaa wiki iliyopita, kutokana
na wadau kuendelea kuchangia tumebakiwa na kiasi cha Sh 67,993,885, kwa
mantiki hiyo busara imeelekeza kuwa nguvu kubwa sasa ipelekwe kwenye
kuwahudumia majeruhi, maana hata tufanyeje kwa wale ambao Mungu kwa
mapenzi yake amewachukua hatuna namna tena ya kuwarudisha.”
Alisisitiza kuwa anapenda kuujulisha umma kuwa leo, atatuma kwa
familia za majeruhi pamoja na madaktari waliojitoa kuwasindikiza
majeruhi kiasi cha Dola za Marekani 20,000, sawa na Sh 44,720,000. Kwa
ujumla baada ya yote hayo kutabakiwa na kiasi cha Sh 23,273,885 huku
wakiendelea kuangalia hali za majeruhi.
Kiasi cha fedha kilichobaki kitaendelea kuwekewa utaratibu kupitia
timu ya wafiwa 4 walioteuliwa na wafiwa wenzao kushirikiana na Serikali
ili kuhakikisha mapato na matumizi ya suala hili yanaeleweka vema kwa
umma.
Pia alitoa rai kwa wananchi kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha
imehitimisha rasmi suala zima la kupokea rambirambi ili ipate muda zaidi
wa kufuatilia mustakabali wa majeruhi walioko haspitalini nchini
Marekani.
chanzo: zanzibar24.
Comments