Mkataba bomba la mafuta wasainiwa.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi na Waziri wa Nishati wa Uganda, Irene Muloni (kushoto) wakisaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga, kwenye hafla illiyofanyika mjini Kampala, Uganda jana. (Picha kwa hisani ya Wizara ya Fedha na Mipango).SERIKALI za Tanzania na Uganda zimetiliana saini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania lenye urefu wa Kilometa 1,443, uliokadiriwa kugharimu zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 3.55.
Mkataba huo ulisainiwa mjini Kampala, Uganda jana baina ya Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi na Waziri wa Nishati wa Uganda, Irene Muloni.

Tukio hilo limefanyika siku chache baada ya Rais John Magufuli wa Tanzania na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, kutia saini tamko la pamoja la kukamilika kwa majadiliano ya vipengele vya mkataba, Ikulu jijini Dar es salaam.
Hafla ya kutia saini Mkataba huo jana, ilifanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Kampala, Uganda na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi zote mbili wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu, wanasheria wakuu wa serikali, wakurugenzi na viongozi wa taasisi mbalimbali zinazohusika katika mradi huo.
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania, unatarajia kuinua uchumi wa nchi hizi mbili. Katika mchakato wa ujenzi wake, zaidi ya watu 10,000 wanatarajiwa kunufaika na ajira.
Hivi karibuni, Rais Magufuli aliuelezea mradi huo kuwa ni mkubwa, kwa kuwa Uganda imegundua shehena kubwa ya mafuta katika eneo la Hoima kiasi cha mapipa bilioni 6.5. Alisema kwamba Tanzania inatarajia pia kupata mafuta Ziwa Tanganyika na Ziwa Eyasi, ambayo yatapitishwa katika bomba hilo.
Akizungumza katika hafla ya kutia saini mkataba wa mradi huo, Waziri wa Sheria na Katiba wa Tanzania, Profesa Kabudi alisema Tanzania inathamini uwepo wa mradi huo na imejipanga kuhakikisha unatekelezwa kwa mafanikio.
Naye Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda, Irene alisema Uganda imeamua kusafirisha mafuta yake kupitia bandari ya Tanga kutokana na Tanzania kukidhi matakwa yenye faida za kiuchumi katika utekelezaji wa mradi huo na kwamba utazinufaisha nchi zote mbili.
chanzo:habarileo.

Comments