Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), imeng’ara katika Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (Ejat) mwaka 2016 kwa waandishi wake watano kunyakua jumla ya tuzo nane.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo za msimu wa nane tangu kuanzishwa kwake ilifanyika jana jijini hapa, zikihusisha vipengele 37 vilivyoshindaniwa.
Washindi kutoka MCL ni Florence Majani aliyeibuka mshindi wa jumla. Pia alinyakua tuzo nyingine mbili; ya utamaduni na ya haki za binadamu na utawala bora.
Sauli Gilliard ameibuka mshindi wa tuzo mbili; ya kilimo na nyingine ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi.
Wengine ni Mussa Juma aliyeshinda tuzo ya uchambuzi wa matukio; Peter Nyanje, tuzo ya utalii na uhifadhi na Kelvin Matandiko, tuzo ya uchumi na biashara.
Akizungumzia ushindi wake, Majani alisema kilichompa ushindi ni jitihada zake za kusoma na kufanya utafiti, pia miongozo na maelekezo kutoka kwa wakuu wake wa kazi.
Majani alisema wakati wote na hata usiku huwa anafikiria ni wazo gani la habari analoweza kulifanyia kazi. Awali, mwandishi wa habari mkongwe, Jenerali Ulimwengu aliyekuwa mgeni rasmi katika utoaji wa tuzo hizo alisema tasnia ya uandishi wa habari si ya watu walioshindwa masomo na kukimbilia huko wakidhani ni shughuli nyepesi.
Alisema shughuli za tasnia hiyo ni muhimu katika maisha ya binadamu kwa sababu inatoa nafasi kwa wanajamii kukusanyika, kuwasiliana na kubadilishana mawazo ili kuondoa tofauti zilizopo miongoni mwao.
Alisema uandishi wa habari ni shughuli ya werevu na umakini wa hali ya juu wa kujua kitu na matokeo ambayo wanajamii hawana nia, hawajui na hawafahamu.
“Kuna muda huwa nasema mwandishi wa habari ni yule mtu anayejiingiza katika mambo ambayo binafsi hayamuhusu,” alisema.
Aliwataka wanahabari kuwa makini katika uandaaji wa habari na kutambua kuwa wanaowafanyia kazi baadhi yao wanajua kuliko wao na kutotumia kigezo cha kuwa katika tasnia hiyo kudhani wanajua kuliko wao.
Pia, aliwataka wanahabari kusoma vitabu na kujifunza kutoka kwa wenzao ili kufanya kazi zao kwa ufanisi.
chanzo:Mwananchi.
Comments