Wakati athari za uhakiki wa watumishi waliogushi vyeti zikiendelea kujionyesha na kuzua tafrani maeneo mbalimbali, Serikali imewataka waajiri katika maeneo yaliyoathirika zaidi na operesheni hiyo kuomba vibali vya ajira vya dharura.
Tangu, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) itoe ripoti ya uhakiki iliyobaini watumishi 9,932 kuwa na vyeti vya kughushi, hali imekuwa tata katika ofisi za umma, kama Shirika la Posta na hospitalini ambako huduma kwa wagonjwa zimeathirika.
Pia, mkanganyiko umeibuka sehemu kadhaa kutokana na baadhi ya wafanyakazi kutajwa katika orodha hiyo wakati wana vyeti halisi, hivyo kuanza kumiminika ofisi za Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kuhoji mustakabali wao, huku wengine wakiamua kutokwenda ofisini hivyo kuathiri huduma.
Akizungumza hali hiyo akiwa bungeni mjini Dodoma jana, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Dk Laurean Ndumbaro alizitaka mamlaka ambazo zimeathirika zaidi na zoezi hilo kuomba vibali vya dharura vya ajira.
“Kuna baadhi ya maeneo yameathirika sana kihuduma na hili zoezi la uhakiki, hivyo watuandikie kuomba vibali vya ajira vya dharura ili huduma zinazotolewa zisiathirike,” alisema. Alisema Serikali itaajiri watu 15,000 kati ya sasa na Juni 30 mwaka huu.
chanzo:Mwananchi.
Comments