Majaa Wilaya ya Magharibi B Unguja pasua kichwa.

Tatizo la uhaba wa gari za kubebea taka linamtoa machozi Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Wilaya Magharibi B, Amour Ali Mussa.

Aidha, Mkurugenzi huyo amekaririwa akisema kuwa hata gari chache walizonazo zinashindwa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na ubovu unaokikabili.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara maalumu ya kamati ya fedha, uchumi na maendeleo ya jamii ya baraza hilo waliyoifanya kukagua majaa mbalimbali yaliyomo katika manispaa hiyo, Mussa amesema kuna taka nyingi zinazozalishwa lakini tatizo ni ukosefu wa gari la kuzibebea.
Amesema kuwa kwa sasa, wanatumia gari moja ndogo ambayo haitoshelezi.
Ili kulipatia ufumbuzi tatizo hilo, Mkurugenzi Mussa amesema manispaa hiyo imeweka mikakati ya kununua gari nyengine lakini inashindikana kutokana na ukosefu wa fedha.
Aidha ameeleza kuwa, kutokana na hali hiyo, ndipo walipoamua kufanya ziara pamoja na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Magharibi B na kamati ya fedha, uchumi na maendeleo ya baraza hilo ili waweze kukaa pamoja na kutafuta njia muafaka ya kutatua tatizo hilo linaloiathiri manispaa na taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi huyo amesema tatizo hilo ni kubwa na linahitaji ushirikiano wa pamoja baina ya taasisi zinazohusika pamoja na wananchi katika ulipaji wa ada za taka zitakazoiwezesha manispaa kupata angalau mapato kidogo yatakayosaidia kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa baraza la manispaa magharibi B Maabadi Ali Maulid, amesema hali ya mazingira hairidhishi na inakaribisha hatari ya kuzuka kwa maradhi ya mripuko.
Amesema uongozi wa manispaa umefanya ziara maalum ya kukagua majaa mbali mbali baada ya kupokea malalamiko ya wananchi juu ya kukithiri kwa taka katika maeneo yao hali inayowaweka katika hatari ya maradhi.
Baadhi ya wananchi wa shehia za Mombasa, Kwa mchina, Magogoni, Kwa mzungu Tomondo, Chochoroni Mombasa pamoja na skuli ya Mwanakwerekwe C, wameeleza kukerwa na majaa yaliyoko kwenye maeneo hayo, na kuliomba Baraza hilo kuziondosha haraka iwezekanavyo.
Na: Takdir Ali, MAELEZO
30 Mei, 2017.
chanzo:zanzibar24.

Comments