Tangu serikali imeanza kuwaondoa wafanyakazi hewa na wenye vyeti feki
kwenye serikali za mitaa na katika mashirika ya umma na wizara baadhi,
mfuko huo haujatikisika kutokana na mfumo mzuri wa utoaji huduma zake.
“Tupo salama, tumeomba serikali ituletee orodha ya majina ya
watumishi wa serikali ambao wameingizwa kwenye orodha ya wafanyakazi
hewa na wenye vyeti feki, sera za mfuko wetu zipo wazi na ndio mfuko
wetu upo imara, ndio umetoa mikopo kwa ajili ya watu mbalimbali
kujiendeleza kielimu na tunatoa mikopo isiyozidi asilimia 75 ya
michango, hata kama wakiondolewa kazini wanaweza kuwa na njia mbadala
kulipa deni hilo,” alisema Kaimu Meneja wa Matekelezo, Voctor Kikoti.
Hadi Aprili mwaka huu, mfuko umetumia zaidi ya Sh bilioni 2.4 kwa
ajili ya kusaidia wanachama 1,438 wanaotaka kujiendeleza kielimu katika
ngazi mbalimbali ndani na nje ya nchi. “Mfuko pia umetoa zaidi ya Sh
bilioni 9.54 kwa ajili ya wanachama 11,744 waliojiunga na mfuko huo kwa
ajili ya mafao ya kujifungua,” alisema Kikoti.
Meneja wa Masoko na Mawasilianowa LAPF, James Mlowe alisema mfuko huo
unaongoza katika kufanya vizuri ukilinganisha na mifuko mingine na
umepata maendeleo makubwa tangu kuanzishwa kwake na hasa tangu Mamlaka
ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA),
ilipofungua milango mifuko yote kutafuta wanachama kutoka sekta
mbalimbali.
Mlowe alisema, kabla ya mfumo huo wa SSRA, ilikuwa ikishughulikana na
wafanyakazi wa serikali za mitaa tu, mara baada ya kufungua milango
hiyo, imeingia kutafuta wanachama kwenye mashirika ya umma, sekta
binafsi na sasa imeingia serikali kuu.
Alisema mfuko huo wa LAPF hadi Aprili Mwaka huu una wanachama
172,000, licha ya uhaba wa ajira katika mwaka uliopita, mfuko huo
ulifaulu kuwasajili wanachama wapya 16,839.
Mfuko huo uliosajiliwa mwaka 1944 na baadaye kuundwa upya nchi ya
sheria Namb 9 ya 2006 inatoa mafao mbalimbali yakiwa ya penseni ya uzee,
ulemavu, warithi pamoja na uzazi, mazishi na mikopo ya elimu. Mengine
ni mafao ya kustaafu na kujitoa pamoja na ndoa, uhamiaji au kutokuwa na
ajira na ugonjwa.
chanzo:Habarileo.
Comments