Ni mkanganyiko. Ndivyo unavyoweza kueleza kuhusu mafanikio ya Wizara ya Afya yaliyoelezwa jana katika hotuba ya bajeti, ikionyesha imepiga hatua kubwa huku Kamati ya Bunge na Kambi ya Upinzani wakibainisha kwamba imekwama kutokana na ufinyu wa bajeti.
Akiwasilisha makadirio hayo ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha upatikanaji dawa kwa kununua, kutunza na kusambaza dawa, vifaatiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Mwalimu akiwasilisha bajeti hiyo, alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 wizara ilitenga Sh251.5 bilioni kwa ajili ya dawa, tofauti na Sh31 bilioni zilizotengwa mwaka 2015/16. Hata hivyo, waziri huyo alisema hadi kufikia Machi, wizara yake ilikuwa imepokea Sh112.2 bilioni sawa na asilimia 45.
Mwalimu alisema kwa ujumla, bajeti ya wizara yake mwaka huu imeongezeka kutoka Sh796,115,856,780 mwaka 2016/17 hadi Sh1,115,608,772,090 sawa na ongezeko la asilimia 40.1.
Lakini Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilisema ongezeko hilo halina tija, kwa sababu hata bajeti ya mwaka unaomalizika Juni 30 imetekelezwa chini ya asilimia 50.
chanzo:Mwananchi.
Comments