Jenerali Dehqan: Tuna uwezo wa kuuza nje makombora na kuongeza kiwango cha uundaji silaha kwa asilimia 100.
Brigedia Jenerali Dehqan amesisitiza kuwa katika teknolojia ya
uundaji makombora, hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefikia
kiwango cha uwezo wa kuunda kombora la masafa yoyote inayotaka, lenye
nguvu ya kusababisha kiwango chochote cha uharibifu inachokusudia na
umakini wa juu kabisa wa kulenga shabaha.
Ameongeza kuwa mafanikio ya
kiulinzi iliyopata Iran ni ya malengo ya kujihami tu kwa ajili ya
kukabiliana na maadui.
Waziri wa Ulinzi wa Iran aidha amebainisha kuwa bei na ubora wa zana
za kijeshi za Iran ni wa namna ambayo licha ya vikwazo vya kidhalimu
ambavyo madola ya Magharibi yaliliwekea taifa hili, zana hizo za ulinzi
zinazozalishwa hapa nchini zinasafirishwa na kuuzwa katika nchi kubwa
kubwa duniani.
Brigedia Jenerali Dehqan ameashiria pia kuongezeka katika kipindi cha
miaka ya karibuni kwa kiwango cha asilimia 100 silaha zinazotengezwa
nchini na kueleza kuwa, leo hii Wizara ya Ulinzi ya Iran ina uwezo wa
kuzalisha silaha na zana zote zinazohitajiwa na vikosi vya nchi kavu vya
jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Waziri wa Ulinzi wa Iran ameongeza kuwa maendeleo yaliyopatikana na
hatua zilizopigwa ni matunda ya jitihada za vijana wenye hima kubwa na
moyo wa kujitolea wa taifa adhimu la Iran.
chanzo: parstoday.
Comments