
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Afisa Mkuu wa doria Pemba, Halfan Amour Juma, amesema kwa sasa Serikali kupitia Idara inayoshuhulika na masuala ya rasilimali za baharini haitakua tayari kuwavumilia wanaozarau sheria za uvuvi na kuchangia uharibifu wa mazingira ya bahari.
Amesema wanajamii pia kwa kushirikiana na taasisi husika wanalo jukumu la kulinda rasilimali za bahari kwa kutoa taarifa sahihi za wavuvi wanaoingia baharini bila ya leseni na kutumia mitengo isiokubalika kisheria, ili kuisaidia Serikali kupata mapato kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao.
Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Ndagoni, Wilaya ya Chake Chake, Masoud Ali Mohd, amewataka wavuvi kuacha kutumia mitego isiokubalika pamoja na kukata leseni kwa wakati, ili kuepuka matatizo wanapokuwa katika shughuli zao.
Aidha amesisitiza kwa wanajamii kupokea elimu wazopatiwa na wataalamu juu ya athari za uvuvi haramu na kuacha tabia ya kuikosesha Serikali mapato ambayo husaidia maendeleo ya nchi .
Nae Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chake Chake, Mfaume Mussa Moh'd, amesema, Idara ya Uvuvi inahitaji kuungwa mkono kutokana na juhudi wanazozifanya, kwani rasilimali za bahari zimekua ni tegemeo kubwa kwa wanajamii na Serikali kwa ujumla,
Amesema, utumiaji nzuri wa rasilimali hizo ni jukumu la kila mwananchi kwani husaidia kwa asilimia kubwa pato la taifa kwa kufuata sheria zilizopo nchini.
Sambamba na hayo amesema kuwa, Jeshi la Polisi litaendelea kutoa ushirikiano na Sekta husika kuwadhibiti watakaopingana na sheria baada ya kufuata taratibu zilizopo na kugundua makosa kwa wahusika watakaofikishwa vituoni.
Jumla ya Wavuvi saba wakaazi wa Shehia ya Ndagoni Kisiwani Pemba, wamefikishwa kituo cha Polisi Chake Chake kwa kushindwa kukata leseni za Uvuvi pamoja na Vyombo vyao wanavyovulia.
Comments