Mbunge
wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), amewatibua wabunge wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) baada ya kuwashangaa jinsi wanavyoisifu Serikali
kutokana na kufuta tozo, kodi na ada katika sekta za uvuvi, kilimo na
mifugo.
Tukio
hilo lilitokea bungeni jana wakati wabunge walipokuwa wakiendelea na
mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa
mwaka wa fedha wa 2017/2018 iliyowasilishwa juzi na Waziri wa Wizara
hiyo, Dk. Charles Tizeba.
Katika
maelezo yake, Mdee aliwaambia wabunge hao kwamba pongezi zao katika
kuondoa tozo hizo hazitakiwi kutolewa kwa kuwa wakulima hawajandaliwa
mazingira mazuri ya kuwanufaisha na kilimo.
Kwa
mujibu wa Mdee, sekta ya kilimo nchini inayohusisha asilimia 65 ya
Watanzania, imekuwa ikishuka kila mwaka badala ya kupanda.
“Nashangaa sana waziri anasimama hapa na kutumia robo tatu ya hotuba yake kueleza masuala ya tozo,” alisema na kuongeza:
“Nawashangaa
pia wabunge wanaosimama na kupongeza kuondolewa kwa tozo na naamini
hizi pongezi zisingekuwapo kama Serikali ingekuwa imeandaa mazingira
mazuri kwa wakulima hao.
“Nimesoma bajeti ya Waziri wa Viwanda, ameeleza kuna viwanda 234 vimesajiliwa kuanza, lakini viwanda vyote viko Dar es Salaam.
“Kwa
tafasiri nyingine ni kwamba wabunge wa Kanda ya Ziwa ambao wanatoka
katika maeneo ya kilimo cha pamba, bajeti hii haikuwaangalia kabisa
ingawa mnasimama hapa na kupongeza.
“Kwa
hiyo, napenda niwashauri wabunge wa CCM ambao ni wapya katika Bunge
hili, kwamba kazi yetu ni kuisaidia Serikali na tunapokuwa tunatoa
pongezi za aina hii wakati tukijua hali ni mbaya, tunaharibu nchi.
“Lazima
wabunge wa CCM msome ilani ya chama chenu ambayo hata mimi wa chama cha
upinzani huwa naisoma ili kupata maarifa na kujua jinsi mlivyojipanga.”
Pamoja
na hayo, Mdee aliishutumu Serikali kwa kushindwa kutoa taarifa ya
upimaji wa ardhi nchi nzima baada ya hoja yake kuungwa mkono na Bunge
mwaka 2011.
Kutokana na maneno hayo, baadhi ya wabunge wa CCM walilazimika kusimama kwa nyakati tofauti na kuomba kumpa taarifa mbunge huyo.
Aliyekuwa
wa kwanza kutoa taarifa ni Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi, ambaye
alimkosoa kwa kusema wabunge wote ni wapya kwa kuwa walipatikana baada
ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.
Mwingine
aliyesimama ni Mbunge wa Nyasa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya, aliyesema
kuipongeza Serikali baada ya kufuta tozo hizo ni jambo la msingi kwa
sababu wabunge wanajua jinsi zilivyokuwa zikiwaumiza wakulima.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Newala, George Mkuchika, alimwambia mbunge huyo
kwamba kila mbunge ana uhuru wa kupongeza katika eneo analoona kuna haja
ya kufanya hivyo.
Wakati
hao wakisema hayo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo),
alisimama na kumwomba Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, amlinde Mdee
kwa kuwa anachokizungumza kinatokana na vitabu vya Serikali.
Kutokana
na hali hiyo, Chenge aliwataka wabunge wasiendelee kutoa taarifa kwa
kuwa mwenye jukumu la kufafanua utendaji wa Serikali ni waziri mwenye
dhamana.
“Kuna utaratibu mmeuanzisha hapa wa mbunge kusimama na kuomba kutoa taarifa na anayepewa taarifa hata kama ni nzuri, anaikataa.
“Lakini
eleweni kwamba anayechangia hapa ni Mdee ambaye maelezo yake yanatakiwa
kujibiwa na waziri mwenye dhamana,” alisema Chenge.
Juzi
Dk. Tizeba wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake, alisema
Serikali imefuta tozo, kodi na ada 108 zilizokuwa kero katika sekta ya
kilimo, uvuvi na mifugo.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments