
Alhaj Dk. Shein, aliyasema hayo katika risala
maalum aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kwa ajili ya
kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu wa 1438 Hijria sawa na
mwaka 2017 Miladiya.
Katika risala yake hiyo, Alhaj Dk. Shein amesema kuwa imekuwa ni
jambo la kawaida kwa baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei za bidhaa
kila unapofika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani jambo ambalo huleta usumbufu
mkubwa kwa wafungaji na wananchi wote kwa jumla.
Hivyo, aliwasihi wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wanaouza bidhaa
zao rejareja na jumla wazingatie wito wake huo na nasaha anazozitoa kwa
kuwahurumia wananchi wenzao kwa kuwauzia bidhaa kwa bei za kawaida,
zilizo nafuu kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanazishukuru neema za
Mwenyezi Mungu na Mola wao atawaongezea Baraka.
Alhaj Dk. Shein, alisema kuwa ni wajibu kujiandaa na kuukaribisha
mwezi wa Ramadhani kwa matumaini na matarajio ya kunufaika na fadhila
zake hivyo, ni vyema juhudi zikaongezwa katika kutoa sadaka kwa kuwapa
wale wanaostahili na wanaohitaji sadaka hizo pamoja na kuwasaidia wenye
uwezo mdogo kutafuta futari na daku katika mwezi huu mtukufu.
Aidha, alieleza kuwa ibada ya funga kwa kawaida ina mafundisho mengi
ikiwa ni pamoja na kuitaka jamii kuishi pamoja, kuheshimiana na
kusaidiana, kustahilimiliana na kuvumiliana, kuwa na subira pamoja na
kuwa na uwezo wa kudhibiti matamanio ya nafsi.
Akieleza athari za mvua za masika, Alhaj Dk. Shein alitoa pongezi kwa
wananchi wote wkwa imani, mapenzi na huruma walizoonesha kwa kuwa
pamoja na wale wote walaioathirika, kwa kuwapa misaada na kuwapongeza
wafanyabiashara na viongozi mbali mbali kwa kushirikiana na Serikiali
katika kuwapa ndugu zao hao misaada muhimu.
Hata hivyo, aliwaahidi wananchi kuwa Serikali itahakikisha michango
na misaada inayotolewa na wananchi, viongozi pamoja na wafanyabiashara
kwa ajili ya wananchi walioathirika na maafa, inawafikia wanaostahiki na
hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaokwenda kinyume na
taratibu zilizopangwa za kufikisha na kuigawa misaaada hiyo.
Alhaj Dk. Shein, pia, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi
kujiepusha kujenga katika sehemu za mabondeni pamoja na maeneo ya njia
muhimu za maji huku akiwataka wananchi kushirikiana na Serikali yao
katika kuvitunza na kuvilinda vianzio vya maji vilivyopo.
Pamoja na hayo, aliwahimiza wananchi pamoja na viongozi wa Manispaa
na Halmashauri kuongeza juhudi katika kudumisha na kusimamia usafi ili
kuepuka miripuko ya maradhi mbali mbali, hasa ya matumbo katika kipindi
hiki cha mvua.
Alisisitiza kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja kwani ana taarifa kuwa
kuna baadhi ya wafanyabiashara wameshaanza kuipuuza miongozo wanayopewa
na wataalamu pamoja na sheria za usafi zilizopo kwani ni vyema ikumbukwe
kuwa mitihani ya maradhi ikitokea watu wa mwanzo ambao kipato chao
huathirika ni wafanyabiashara.
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imekuwa ikiimarisha mipango na mikakati
iliyokuwepo ya kujikinga na kukabiliana na maafa pamoja na kufanya
marekebisho ya sheria iliyokuwepo na kuziimarisha taasisi husika.
Kwa mujibu wa maelezo ya Alhaj Dk. Shein, hivi Serikali inaadaa
mpango wa kuliondoa tatizo la mafuriko katika eneo la Mwanakwerekwe na
sehemu nyengine kupitia Awamu ya Pili ya Mradi wa ZUSP sambamba na
kujenga barabara imara katika barabara ya Kibonde Mzungu ili iweze
kupitika bila ya shida katika misimu yote.
Alhaj Dk. Shein, alitoa shukurani zake kwa wananchi wote kwa
kuendelea kushirikiana na Serikali katika kudumisha umoja na mshikamano
uliopo na kuwataka kuendeleza utamaduni wao wa kuishi kwa pamoja bila ya
kubaguana kwa dini ama kabila.
Aliongeza kuwa mashirikiano ya pamoja yamewezesha kuongeza kasi ya
ukuaji wa uchumi ambapo katika mwaka uliopita, uchumi ulikuwa kwa
asilimia 6.5 na mfumko wa bei ulibaki katika tarakimu moja, asilimia 5.7
sambamba na kupiga hatua katika ukusanyaji wa mapato.
Pia, Alhaj Dk. Shein, aliikumbusha Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na
Mazingira iendeleze utaratibu kwa kusambaza maji katika Mwezi huu
mtukufu wa Radhamani, katika maeneo mabli mbali ambayo huduma za maji
safi salama huwa zina upungufu na kuwataka wananchi kushirikiana na na
wafanyakazi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), ili kazi ya kusambaza
maji ifanyike vizuri.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
chanzo: zanzibar24.
Comments