Dr Mabodi: nitalinda mali za CCM kwa Gharama yoyote.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,  Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” amesema atalinda na kusimamia kikamilifu mali na miradi mbali mbali inayomilikiwa na chama hicho ili iwanufaishe wananchi wote badala ya watu wachache wanaojimilikisha baadhi ya  rasilimali hizo kinyume cha sheria.

Msimamo huo ameutoa wakati akikagua shamba la CCM lenye zaidi ya hekta 200 huko katika Kijiji cha Kilombero Wilaya Kaskazini “B” Unguja, alisema CCM haiwezi kufikia dhamira yake ya kuimarika kiuchumi endapo kama kuna baadhi ya watu wanaotumia rasilimali hizo kwa maslahi binafsi.


Alisema lengo la CCM kupitia mabadiliko ya muundo wa taasisi hiyo yaliyofanyika hivi karibu ni kuhakikisha rasilimali zinatumika vizuri na kwa maslahi ya wengi kwa lengo la kufikia dhamira chama hicho kujitegemea kiuchumi.

Dkt. Mabodi alisema CCM itasimamia Utekelezaji wa Ilani yake ya  Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kama ilivyowahidi wananchi kwa kuhakikisha inaondosha mianya yote ya ubadhirifu  wa mali za chama hicho.

Ni msafara wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala na baadhi ya wananchi wakiongozwa na Viongozi wa CCM Wilaya ya CCM Kaskazini “B”, wakikagua shamba hilo.
Hata hivyo alifafanua kwamba atashirikiana kikamilifu na chombo kilichopewa dhamana ya kusimamia rasilimali zote za CCM  ambacho ni Baraza la Wadhamini kwa lengo la kukagua mali hizo na kutatua kasoro zilizopo ili kuongeza ufanisi ndani ya taasisi hiyo.

“ CCM tuna mashamba ya kilimo cha kisasa hivyo natoa wito kwa vijana wetu badala ya kudai ajira kutoka serikali na katika makampuni pia watumie fursa za kilimo kujiajiri wenyewe kwani nchi yetu ina soko kubwa la mazao ya kilimo hasa katika Mahoteli ya kitalii.”, alitoa Wito kwa Vijana Dkt. Mabodi.

Naibu Katibu Mkuu huyo akizungumzia malalamiko ya baadhi ya wamiliki wa maeneo yaliyopakana na shamba hilo wanaodai kumiliki baadhi ya miti ya miembe na vipande vya ardhi katika eneo hilo, aliwaruhusu waendelee kuvuna maembe hayo huku CCM ikijadili njia bora ya kumaliza tatizo hilo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala akishauriana masuala mbali mbali na baadhi ya wananchi wakiwa ndani ya shamba hilo.
Pia Dkt. Mabodi alisifu juhudi za Wasisi wa ASP walionunua shamba hilo kwa njia ya kuchangishana fedha ili litumike kwa ajili ya makaazi ya wananchi waliokuwa hawana sehemu za kuishi baada ya ardhi zao kudhurumiwa na utawala wa kimabavu uliotawala Zanzibar kabla ya Mapinduzi ya Mwaka 1964.

Aliwasihi vijana wa sasa kufuata nyayo za waasisi hao kwa kuhakikisha wanalinda na kuanzisha vitega uchumi  vipya na rasilimali za kudumu za CCM ili viweze kubaki kama kumbukumbu ya kujivunia na kuvinufaisha vizazi vijavyo.

Aidha Dkt. Mabodi aliwataka wafugaji wa kijiji hicho kuacha tabia za kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima hasa wa Zao la mpunga, kwani kufanya hivyo ni kuchochea migogoro isiyokuwa ya lazima.

Pia aliuagiza uongozi wa CCM Wilaya hiyo kuhakikisha katika shamba hilo hapajengwi nyumba na miradi ya kudumu ya watu binafsi sambamba na kulinda wananchi wanaoishi katika eneo hilo mpaka pale chama kitakapokaa na kufanya maamuzi ya mwisho yatakayojali utu na haki za wananchi hao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji hicho, walisema matarajio yao baada ya ziara hiyo ni kutatuliwa kwa haraka changamoto zinazowakabili.
Moja ya maeneo ya wananchi yaliyolimwa mpunga yaliyopo katika shamba hilo.
Naye mkaazi wa kijiji hicho , Juma Vua aliwasihi viongozi wa Chama na Serikali kuiga utamaduni wa Naibu Katibu Mkuu huyo Dkt. Mabodi kwa kuwatembelea wananchi katika maeneo yao ili kujionea kero na changamoto zinazowakabili kwa lengo  la kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Shamba hilo ambalo ni miongoni mwa urithi wa waasisi wa  Afro Shiraz Party(ASP) walionunua rasilimali hiyo toka mwaka 1953 kutoka mikononi mwa mmoja wa viongozi wa kisultani kwa ajili ya wananchi waliokuwa wakiishi bila ya makaazi ya kudumu waishi katika eneo hilo  baada ya kunyang’anywa ardhi yao na utawala wa wakati huo.
chanzo:zanzibar24.

Comments