RAIS John Magufuli ameendelea kupongezwa kutokana na kuchukua hatua kutokana na`madudu’ yaliyoibuliwa kwa Tume aliyoiunda kuchunguza makiniakia katika mchanga wa dhahabu uliokuwa unasafirishwa kwenda nje ya nchi.
Miongoni mwa waliopongeza ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa zamani, Andrew Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi, wachimbaji wadogo wa mgodi wa dhahabu Mwakitolyo wilayani Shinyanga, Jumuiya mbalimbali za chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini pia wasomi na viongozi na makada wa vyama vya siasa, vikiwemo vya upinzani.
Chenge, akizungumza alimpongeza Rais Magufuli kwa hatua ya kuchunguza makinikia na kubaini madudu yaliyojificha, akisema suala hilo lilishaibuliwa tangu zamani kupitia tume ya Jaji Mark Bomani, lakini tatizo lilikuwa utekelezaji wa mapendekezo ya kamati hiyo.
Aliyasema hayo katika viwanja vya Bunge Dodoma jana wakati alipozungumza na gazeti, baada ya ripoti ya uchunguzi wa makinikia hayo iliyowasilishwa rasmi hivi karibuni kwa Dk Magufuli.
Mara baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa watendaji wote wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa kile kilichodaiwa kushindwa kujenga kinu cha kuchenjulia makinikia tangu mwaka 2010, licha ya sera ya madini ya mwaka 2009 kuagiza.
Alisema makinikia ni mali ya Watanzania, hivyo ilikuwa ni lazima wahoji na hatimaye kupatiwa ukweli. “Ingawa wengine wanaamini kwamba tunaibiwa, kweli wengine hawaamini.
Lakini pia wakizipiga zile hesabu mimi ukiniambia kwamba ni Sh trilioni ndio tumepata hasara nakataa kwa sababu I know it (najua)… lakini nadhani kuna mahesabu wameyakosea,” alisema Chenge.
Awali, Chenge ambaye ana majina mengi ya utani ikiwemo mzee wa vijisenti na Mtemi, aligoma kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu suala hilo na kuishia kusema tu kwamba kwa kilichotokea Watanzania wanatakiwa kukumbuka historia.
“Sina comment nawaambieni. Yawezekana ninyi hamkumbuki historia ripoti ya Bomani ilitoa mapendekezo kwa serikali ione uwezekano wa kufanya smelting ‘uchenjuaji’ hapa nchini,” alisema.
Alisema pamoja na historia kuonesha kuwa suala hilo lilishawahi kuibuliwa, anajua wapo watu watahoji kwanini hatua hazikuchukuliwa kipindi kile lakini muhimu ni kwamba sasa Watanzania wamejua ukweli.
Alipoulizwa kuhusu madai ya kuwa Mwanasheria Mkuu katika kipindi cha miaka ya 1990 na 2000, alisema yeye ameshazoea kubebeshwa mizigo mingi, ingawa kipindi hicho kinachodaiwa kuhusika na suala hilo la makinikia hakuwa mwanasheria mkuu.
“Ukiniambia nilikuwa mwanasheria mkuu kipindi kile ninachosema ni kwamba Chenge anabeba mengi huwa nawaambia Watanzania basi Chenge ana akili sana. Maana kama wote wale baraza la mzee Mwinyi, lakini naonekana mimi,” alisema.
Alikiri kwa upande wake kufahamu mambo mengi kwani amekuwepo kwenye awamu tofauti hadi ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, na kubainisha kuwa amesomea mambo ya mikataba ya madini na petroli. Lakini watu hawajui, unadhani mie nayajuaje haya?.
Alisema Dk Magufuli aliamua kuwakumbusha Watanzania kuhusu mapendekezo ya Bomani na kubainisha hayo yaliyoibuliwa. “Baada ya hapo sasa muulizane inawezekana au haiwezekani hilo sasa ni suala tofauti, je tumejielekeza huko?” alihoji.
Wachimbaji roho kwatu Wakati Chenge akiyasema hayo, wachimbaji wadogo wa mgodi wa dhahabu Mwakitolyo wameelezea kufurahishwa na kazi nzuri ya tume ya kuchunguza mchanga wa madini iliyoundwa na Rais Magufuli kwa kufichua `madudu’ yaliyokuwa yanatendeka katika sekta ya madini nchini.
Walidai kuwa wangeshangaa kama wangesikia kuwa kamati hiyo katika ripoti yake, ingesema kuwa hakuna dhahabu iliyokuwa ikiondoka nchini. Walidai kuwa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakishuhudua baadhi ya watumishi ndani ya migodi mbalimbali, wakifumua vifungashio vya makontena yenye mchanga unaopelekwa nje na kuchota kwa lengo la kuwauzia wachimbaji wadogo, kwa lengo la kujipatia fedha.
Waburuzwe kortini Aidha, pamoja na kukunwa na hatua zilizochukuliwa na Rais Magufuli, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani Kilimanjaro, umeiomba Serikali kuwafikisha mahakamani, viongozi wote wanaotenguliwa kwenye nafasi zao kutokana na kosa la ubadhirifu wa mali za umma.
Mwenyekiti wa Umoja huo Kilimanjaro, Juma Raibu alisema hayo jana wakati akiunga mkono tamko la UVCCM -Taifa, la kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa uzalendo wa hali ya juu alionao kwa taifa.
Alisema wanaunga mkono tamko hilo lililotolewa juzi na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Shaka Hamidu Shaka, kutokana na juhudi na jitihada anazozifanya Rais Magufuli huku akizingatia maagizo ya chama na maelekezo ya Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Alisema, Machi 29, mwaka huu, Rais aliunda Tume ya kuchunguza mchanga wa madini ili kujua taifa linapoteza kiasi gani, na Mei 23 kamati hiyo iliwasilisha ripoti pamoja na maoni na mapendekezo ambayo UVCCM imeyaunga mkono kupitia tamko lililotolewa na Shaka na kumpongeza Rais kwa hatua alizochukua kulinda haki na maslahi ya umma.
Vijana wengine wa umoja huo mkoani Dodoma, pia wamesifu na kumpongeza Rais Magufuli kwa kufanya mambo mengi makubwa ndani ya kipindi kifupi cha utawala wake, ukiwa ni pamoja na kusimamia ustawi wa nchi, kurejesha nidhamu ya utendaji Serikali, kudhibiti mianya ya rushwa na mambo mengine yaliyokuwa yanafanywa kiholela.
Akisoma tamko hilo la Vijana jana, Katibu wa UVCCM Mkoa wa Dodoma, Asia Halamga alisema hatua hizo zimefurahiwa na wananchi wengi wanaoridhishwa na mambo makubwa yanayofanywa na Rais Magufuli.
“Pia Rais Magufuli ndani ya kipindi kifupi serikali yake imeweza kununua ndege ili kuipa msukumo sekta ya utalii na kuliinua Shirika la Ndege, ameweka azma ya kuanza ujenzi wa reli ya kisasa, kuweka malengo ya kisera na kutaka kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda kuelekea uchumi wa kati.
Pia amehamishia makao makuu ya Serikali Dodoma baada ya kushindikana kwa miongo minne,” alisema. Aliongeza kuwa, amekuwa mfano bora katika usimamizi, umakini na ushupavu wa kuongoza wananchi wake huku serikali yake ikiimarisha huduma za jamii, kukusanya mapato kwa uhakika na kuwachukulia hatua za kisheria watendaji wote wazembe bila kuwaonea aibu.
UWT nao wanena Nao Umoja wa Wanawake Nchini (UWT), umesifu hatua iliyochukuliwa na Rais Magufuli katika sekta ya madini mara baada ya kupokea taarifa ya ubadhirifu uliofanyika katika usafirishaji wa mchanga wenye madini nje ya nchi.
Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Masaburi alisema kitendo alichokionesha Rais Magufuli ni cha kishujaa na kinastahili pongezi. “Tumeibiwa rasilimali zetu kwa miaka mingi sana na mpaka sasa bado inaonesha bado wizi unaendelea, lakini Rais Magufuli ametengeneza mfumo mzuri wa uwajibikaji anastahili pongezi kubwa,” alisema Mama Masaburi.
Wengine waliopongeza ni pamoja na wasomi, wachumi na wanasiasa mahiri akiwemo Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo.
Imeandikwa na Halima Mlacha (Dodoma), Flora Mwakasala (Moshi), Sifa Lubasi (Dodoma), Regina Mpogolo (Dar es Salaam).
chanzo:Habarileo.
Comments