
Mvua hizi zinazoendelea kunyesha zimeathiri maeneo mbali mbali hasa
katika kisiwa cha Pemba. Maeneo hasa yalioathiriwa yakiwemo Vijiji vya
Mbuyuni, Mwambe, Uweleni, Makombeni, Ukutini, Kendwa, Vitongoji,
Chamanangwe na maeneo mengine katika Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba.
Pia zimeathiri miundombinu, majengo ya wananchi na ya Serikali.
Pamoja na juhudi zinazochukuliwa na Serikali za kuendelea kufanya
tathmini ya kitaalam juu ya kubaini athari kubwa zinazotokana na mvua
hiyo. Chama cha Mapinduzi Zanzibar kinaishauri Serikali na Asasi
nyengine kwa msisitizo mkubwa zichukue hatua za haraka za kupeleka
misaada ya dharura kwa Wananchi wa maeneo yaliyopata na athari za mvua
hiyo ili kunusuru kutokea kwa majanga mengine yakiwemo njaa, maradhi ya
miripuko n.k.
CCM inawaomba wananchi wa Kisiwa cha Pemba na maeneo mengine
kuendelea kuwa na subira, utulivu katika kipindi hichi kigumu,
huku Chama Cha Mapinduzi kwa kushirikiana na Serikali zikiendelea
kushughulika na kutafuta ufumbuzi wa haraka juu ya kutatua matatizo
hayo ili wananchi warejee katika hali zao za kawaida.
Aidha Chama cha Mapinduzi kinawasihi Wahisani, Marafiki wa ndani na
nje ya Nchi, watu wenye uwezo popote walipo kujitokeza kuchangia misaada
ya Kibinadamu katika athari hizi za mvua zilizojitokeza.
Mwisho, tunawaomba wananchi wa maeneo mbali mbali hasa wale wanaoishi
katika maeneo ya hatarishi kuchukua tahadhari, sambamba na kufuata
kanuni za kiafya ili kuepukana na majanga mengine.
Comments