Ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, katika halmashauri ya jiji hili mwishoni mwa mwezi uliopita limeacha mgogoro kati ya meya wa jiji , James Bwire na mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Kiomoni Kibamba.
Wakati akihutubia wakazi wa kata ya Mahina jijini hapa Aprili 28 mwaka huu baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mkazi wa mtaa wa Kagomu, Gadison Kagiri kwamba meya huyo amepora eneo lililotengwa na halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na shule ya Serikali, Lukuvi alimwagiza mkurugenzi wa halmashauri ya jiji, Kibamba kushughulikia suala hilo.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika mtaa wa Kagomu kata ya Mahina juzi, Bwire ambaye pia ni diwani wa kata hiyo (CCM), alithibitisha kuwepo kwa mgogoro huo, huku akidai mgogoro huo unatokana na msimamo wake wa kuziba mianya ya ufisadi katika halmashauri hiyo.
Hata hivyo, mkutano huo ambao uliandaliwa kwa ajili ya kupata ufafanuzi kuhusu tuhuma zinazomkabili Bwire uliingia dosari baada ya mwenyekiti wa mtaa wa Igelegele katika kata hiyo, Dunkan Nyamgocho kuibuka na kudai hadharani kwamba Bwire ni mwongo, kauli ambayo ilisababisha meya huyo kuagiza mwenyekiti huyo kunyang'anywa kipaza sauti.
Licha ya dosari hiyo, Kibamba naye amethibitisha kuwepo kwa mgogoro huo na kwamba ataendelea kusimamia sheria na maelekezo ya viongozi wa juu serikalini.
Amesema kuwa anatarajia kulifikisha suala hilo kwa mkuu wa wilaya, Mary Tesha na mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella ili wasaidie eneo hilo kurejeshwa.
Comments