Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto imefanikiwa kuwarejesha skuli watoto 5,067 na kuwapeleka elimu mbadala.

Image result for elimu mbadalaMKURUGENZI wa Usalama na Afya Kazini Suleiman Khamis Ali amesema, Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto imefanikiwa kuwarejesha skuli watoto 5,067 na kuwapeleka elimu mbadala kwa wale waliofikia umri wa miaka 17, ambao wametolewa katika ajira za watoto na waliokuwa katika hatari wa kuingia katika ajira hizo.

Aliyasema hayo wakati akiwasilisha ripoti ya ajira za watoto na walio katika mazingira magumu kwa Kamati ya Maendeleo ya Wanawake,
Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi, katika ukumbi wa Wizara ya Katiba na Sheria Pemba.

Amesema kuwa, kati ya watoto hao, jumla ya watoto 1,188 wametolewa katika ajira za watoto wakiwemo wanawake 479 na wanaume 709, ambapo jumla ya 3,879 walikuwa katika hatari ya kuingia katika ajira za watoto.

Ameeleza kuwa, watoto hao 5,067 walifikiwa na mradi wa ‘Fighting Against Child Labour in Zanzibar’ ambapo serikali ikishirikiana na save the Children chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya (EU), ambao ulitekelezwa kwa muda wa miaka mitatu, ukiwa na lengo la kupunguza ajira za watoto Zanzibar kwa shehia 50.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi Ali Suleiman Ali, amewataka wazazi kuwapeleka watoto skuli, ili kuweza kupata elimu itakayoweza kuwasaidia katika maisha yao baadae.

 Nae Sheha wa shehia ya Micheweni Juma Dawa Mshindo alisema kuwa, kwa sasa hali inaridhisha ukilinganisha na kipindi cha nyuma, kwani watoto wanakwenda skuli na wanaporudi ndio wanakwenda kubanja kokoto.

Katika ziara hiyo pia iliwasilishwa ripoti ya utendaji wa Idara ya Ajira kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu na Mkurugenzi wa Ajira Ameir Ali Ameir na kusema kuwa, Idara imesajili vijana 731, ambapo jumla ya vijana 170 wamepata fursa ya ajira nje ya nchi.

Comments