Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ufaransa, Waziri wa Ulinzi wa Marekani jana Alkhamisi alifanya ziara ya siku moja nchini Misri na kuonana na Rais Abdul Fattah el Sisi na Sedki Sobhi, waziri wa ulinzi wa Misri. Pande mbili zimezungumzia ushirikiano wa nchi zao katika masuala ya kijeshi na kiusalama hususan hali ya mkoa wa Misri wa Sinai Kaskazini.
Wakuu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani wamedai kuwa wana wasiwasi na magaidi wa Daesh (ISIS) wanaozidi kujipenyeza nchini Misri kutokea nchi jirani ya Libya.
Ofisi ya Rais wa Misri imetoa tamko na kusema kuwa, katika mazungumzo hayo, Rais Abdul Fattah el Sisi ametaka uhusiano wa kijeshi wa nchi hizo mbili uimarishwe, na waziri wa ulinzi wa Marekani naye amesisitizia jambo hilo hilo.
Safari ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani nchini Misri imefanyika wiki mbili baada ya Rais wa Misri kutembelea Marekani.
Kila mwaka Marekani inaipatia Misri msaada wa karibu dola bilioni moja na nusu ambapo dola bilioni moja na milioni 300 zinatumika katika masuala ya kijeshi huko Misri.
chanzo:parstoday.
Comments