Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu ametoa agizo hilo bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM).
Waziri Ummy amesema suala la mashirika na taasisi za umma kujiunga na
NHIF halina mjadala, ni suala la lazima na hivyo ni vema taasisi zote
na mashirika ya umma yakajiunga na mfuko huo haraka iwezekanavyo.
Amesema, kuna mashirika na taasisi za serikali ambazo hawajajiunga na
NHIF, hivyo serikali inaendelea na mazungumzo na taasisi hizo ili
kuhakikisha kuwa wanafanya hivyo mara moja.
Akijibu swali la msingi la mbunge huyo aliyehoji ni taasisi na
mashirika ya umma mangapi yamejiunga na NHIF, Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla
alisema hadi kufikia Machi, mwaka huu idadi ya wanachama katika mfuko
huo ni 792,987 kutoka wanachama 474,760 mwaka 2012.
Alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, mfuko huo umefanya
maboresho mbalimbali ya vitita vya mafao na namna ya kuchangia kwa
makundi mbalimbali ya jamii.
"Maboresho haya yamewezesha kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya
wanachama walio katika mfumo huu wa bima ya afya nchini na kufanya
wanufaika kufikia asilimia nane. Hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana
idara za serikali, taasisi na mashirika ya umma zinazotumia huduma za
bima ya afya za NHIF zimefikia 307. Idadi hii imetokana na jitihada za
makusudi za kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya kwa
watumishi wa umma," amesema.
Amesema mashirika, taasisi na idara za serikali ambayo hayajajiunga
na mfuko huo yapo 23 yakiwemo Mamlaka ya Mapato (TRA), Benki Kuu (BoT),
Shirika la Umeme (Tanesco), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari(TPA), PSPF, LAPF, PPF, Ewura, NCA na GEPF.
chanzo:Habarileo.
Comments