Hayo yamesemwa bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokuwa akiongezea majibu
yaliyotolewa na Naibu Waziri, Dk Khamis Kigwangalla.
Ummy amesema mgonjwa wa kifua kikuu akiachwa bila ya kupata huduma ana uwezo wa kuwaambukiza watu 20 kwa mwaka.
Amewaomba wabunge kuona umuhimu wa kuwahamasisha wananchi wao kuhusu ugonjwa huo wanapokuwa majimboni.
Vilevile, alisema ili kukabiliana na hali hiyo, serikali imeweka
mpango kwa kila mjamzito na mtoto wa umri wa miaka chini ya mitano
kupimwa Kifua Kikuu na Ukimwi ili kupata takwimu sahihi.
Katika swali hilo, Mbunge wa Busanda, Lolesia Bukwimba (CCM), ambaye
alitaka kujua kama serikali inafahamu tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu
limeathiri watu wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini na
wale wanaoishi kandokando na maeneo ya wafugaji.
Pia, alihoji serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kupambana na
ugonjwa huo na silicosis hasa katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji
wa madini.
Akijibu swali hilo, Dk Kigwangalla amesema Tanzania inafahamu uwepo
wa magonjwa ya kifua kikuu na silicosis katika maeneo ya wachimbaji.
Naibu Waziri amesema kwa upande wa kifua kikuu inakadiriwa kuwa
ukubwa wa tatizo hilo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na hali halisi
katika maeneo mengine.
Kuhusu silicosis, amesema kumekuwepo na ripoti za wagonjwa ambao ni
wachimbaji wadogo wachache katika hospitali za serikali ikiwemo
Kibong'oto.
Hata hivyo, alisema serikali kupitia halmashauri zilizo katika maeneo
ya migodi imeanza kuweka mikakati ya kudhibiti magonjwa hayo kwa
kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu
na Malaria.
chanzo:Habarileo.
Comments