Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha,
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Onesmo Lyanga, alisema pikipiki nyingine
mbili zilifanikiwa kukimbia.
Lyanga akielezea juu ya tukio hilo, alisema limetokea Aprili 2, mwaka huu saa 6:00 mchana Mwembe Muhoro Wilaya ya Rufiji.
“Siku ya tukio askari walipata taarifa kuwa kulikuwa na pikipiki tatu
zikitokea Kibiti kwenda mikoa ya Kusini zikiwa zimebeba watu watatu
kila moja huku miongoni mwa pikipiki hizo kati yake mbili wamebebwa watu
waliovaa hijabu,” alisema Kamanda Lyanga.
Alisema askari wa barabarani walipewa taarifa katika kizuizi cha
Mparange na kuwasimamisha ili wawahoji, lakini walikataa na kupita
ambapo waliwajulisha wenzao kwenye kizuizi cha Ikwiriri, lakini
walikaidi kusimama kupita kwa kasi.
“Baada ya hapo walifika katika kizuizi cha Ikwiriri, lakini bado
walikaidi kusimama na kuendelea kukimbia ndipo walipofika kituo cha
Mwembe Muhoro hata hivyo hawakusimama na askari waliokuwa doria wakiwa
kwenye gari waliwafuatilia na wakavuka Daraja la Mkapa na waliwapa onyo
kwa kupiga risasi hewani,” alifafanua.
Alisema baada ya hapo watu hao waliruka kwenye pikipiki na kuanza
kukimbilia msituni na ndipo askari walipowapiga risasi za miguu na
kiunoni na kuwakamata.
“Majeruhi hao walijulikana ni wanaume hata hivyo majina yao
hayakuweza kufahamika na walikuwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili
MC 272 BLW aina ya Boxer yenye rangi nyeusi ambapo watu hao
wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu kwa mwonekano wao walijaribu kuwawahisha
Hospitali ya Misheni ya Mchukwi,” alieleza kamanda.
Alisema walipofikishwa hospitali daktari alithibitisha kuwa watu hao
wamekufa ambapo hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika huku
pikipiki nyingine mbili zilitoroka na kuelekea Mkoa wa Lindi na taarifa
zimetolewa polisi ili wawakamate.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu wanaposimamishwa na askari polisi
badala ya kujaribu kutoroka na kwa sasa jeshi hilo limeimarisha doria
katika kukabiliana na uhalifu.
chanzo:Habarileo.
Comments