Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam, kwa
niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Felix Ngamlagosi, Meneja
Mawasiliano na Uhusiano, Titus Kaguo alisema bei ya mafuta ya taa
imepanda kwa Sh saba sawa na asilimia 0.36 wakati bei ya dizeli imepanda
kwa Sh 12 kwa lita sawa na asilimia 0.63.
Kaguo alisema kutokana na kupanda huko kwa bei hizo, mafuta ya taa
sasa yatauzwa Sh 1,858 kutoka Sh Sh 1,852 huku dizeli ikuzwa Sh 1,925
kutoka Sh 1,913 kwa lita.
Alifafanua kuwa mabadiliko hayo kwa kiasi kikubwa yametokana na
mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia, mfumuko wa bei na
gharama za usafirishaji ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Hata hivyo, alisema kwa upande wa mafuta yanayoshushiwa mkoani Tanga
pamoja na kwamba hakuna meli iliyoshusha mzigo wa mafuta katika bandari
hiyo, nako bei ya mafuta kuanzia leo itapanda kwa aina zote tatu za
mafuta kwa Sh saba.
Alisema hali hiyo imetokana na hatua iliyochukuliwa na Ewura katika
kuwasaidia wafanyabiashara wa mafuta kupambana na tatizo la mfumuko wa
bei kwa kuwaongezea Sh tatu katika faida wanazopata.
Alisema Watanzania wanaweza kufuatilia bei za mafuta kulingana na eneo au mkoa wanaotoka ama kwenda kupitia namba *150*#.
Alisisitiza kuwa kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta
ya petroli kwa bei ya ushindani ili mradi tu bei hizo ziwe chini ya bei
kikomo zilizotolewa na mamlaka hiyo baada ya kuzikokotoa kwa mujibu wa
kanuni ya kukokotoa bei za mafuta.
Aliwakumbusha wamiliki wa vituo vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa
za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei hizo za
mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni.
chanzo:Habarileo.
Comments