‘Wataalamu wa kusimamia vihatarishi hawatoshi’.

Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Mohamed MtongaSERIKALI imesema kama nchi itakuwa na wataalamu wa kutosha wenye ujuzi wa kusimamia vihatarishi, taifa litaokoa fedha nyingi kutokana na matukio ya hatari ambayo yangeweza kuepukwa ikiwemo manunuzi hewa, mfumuko wa bei, wizi na upotevu wa mali za umma.
Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Mohamed Mtonga, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki katika mahafali ya kwanza ya Taasisi ya Usimamizi wa Vihatarishi Tanzania (IRMT) ambayo wahitimu 12 walitunukiwa vyeti vyao.

Mtonga alisema nchi ina uhaba mkubwa wa wataalamu wa masuala ya usimamizi wa vihatarishi na taasisi hiyo ina nafasi nzuri ya kupunguza uhaba huo.
“Napongeza jitihada za uongozi wa taasisi kwa kuweza kuanzisha program ya mafunzo ya weledi ya usimamizi wa vihatarishi yanayohusiana na taasisi za fedha , ikilenga rasmi kuinua kiwango cha taaluma cha wataalamu wa taasisi za fedha na serikali ili waweze kumudu kusimamia vihatarishi kwa umahiri na bidii,” alieleza.
Alisema katika kuzingatia mabadiliko ya sera za kiuchumi kitaifa na kimataifa inawalazimu waliohitimu kuelewa kuwa serikali haibebi jukumu la kuajiri bali inaweka tu mazingira mazuri na kutoa mwongozo utakaowezesha elimu inayopatikana itumike ipasavyo.
Kutokana na hilo, aliiomba taasisi hiyo kutoa mafunzo yatakayowawezesha wataalamu kuwa na mtazamo wa kujiajiri kuliko kutegemea kuajiriwa na taasisi au mtu mwingine.
Aidha, alisema serikali itasaidia taasisi hiyo ili iweze kukua na kujiendesha kwa ufanisi kwa kujikita katika kuboresha taaluma ya usimamizi wa vihatarishi katika ngazi zote.
chanzo:Habarileo.

Comments