Wanafunzi 5 wa kike watoroka Ukerewe.

Mkuu wa wilaya ya Ukerewe, Estomiah Chang’ah WANAFUNZI watano wa kike wa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, wametoweka kwa nyakati tofauti katika mazingira yenye utata na kwamba hadi sasa hawajulikani walipo.

Taarifa zilizolifikia gazeti ili kwa nyakati tofauti zinaonesha wanafunzi hao wa elimu ya msingi na sekondari walitoweka kati ya Oktoba mwaka jana na Februari mwaka huu.

Hata hivyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Estomiah Chang’ah amehusisha tatizo hilo na wanafunzi wanaopata mimba na kisha wazazi hutoa visingizio vya wanafunzi hao kupotea.

Wanafunzi watatu ambao ni Consolata Chibuga wa darasa la saba Shule ya Msingi Kakerege na Judis Kayumba wa darasa la pili Shule ya Msingi Nakoza na Nisawa Abubakar wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Nakatungulu wametoweka tangu Oktoba 17, mwaka jana.

Wakati huo, Muhailwa Dotto ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne wa Shule ya Msingi Mulezi alitoweka Januari 29, mwaka huu na Gloria Majaliwa wa darasa la pili Shule ya Msingi Kakerege alitoweka Februari 25, mwaka huu.

Juma Mazigo anasema mtoto wa shemeji yake, Gloria (13), ametoweka tangu Februari 25, mwaka huu na hadi sasa hajulikani alipo.

Alisema siku hiyo, Gloria alitoroka na kulala kwa shangazi yake, Lucia Nyakalonge baada ya mkewe ambaye ni mama yake mdogo, kutishia kumpiga kwa sababu ya kukaidi maelekezo yake na siku iliyofuta aliaga kurudi nyumbani, lakini akaenda kusikojulikana.

Walimu wakuu wa shule hizo wamethibitisha wanafunzi hao ni watoro wa muda mrefu huku Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kakerege, Diamond Msita anasema juhudi za kuwatafuta wanafunzi hao ili warudi na kuendelea na masomo zinaendelea.
chanzo:Habarileo.

Comments