Wamiliki mabasi wasitisha mgomo.

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani (TABOA) kwa pamoja na Chama cha Wasafirishaji wa Daladala (UWADAA) na wenye malori (TAT), wamekubali kusitisha mgomo uliopangwa kuanza leo baada ya kukubaliana na serikali kuhusu kuwepo kwa marekebisho ya Rasimu ya Kanuni ya Usafirishaji.

Kwa mujibu wa wamiliki hao, wanahitaji rasimu ya kanuni hiyo itambue na kutenganisha makosa yanayofanywa na dereva na yale yanayomhusu mmiliki, lakini pia iandikwe kwa lugha ya Kiswahili.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Gilliard Ngewe alisema usitishwaji wa mgomo huo umekuja baada ya kuwepo kwa majadiliano ya muda mrefu kati ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na wadau hao wa usafirishaji.

“Baada ya vyama hivyo kutangaza kuwepo kwa mgomo kuanzia kesho (leo), waziri alikutana na wahusika hao kuanzia jana asubuhi na kujadiliana kuhusu kanuni hizo akiwashirikisha pia Sumatra na wameafikiana mambo mawili makubwa,” alibainisha Ngewe.

Alisema katika majadiliano na waziri, wamekubaliana kuwa ndani ya siku 14 rasimu yote iandikwe kwa Kiswahili na wadau wa usafirishaji kutoka vyama hivyo waipate na kutoa michango yao kwa ufasaha kwa Kiswahili. Jambo la pili walilokubaliana ni kanuni hizo kutenganisha makosa ya wamiliki wa mabasi na makosa yafanywayo na madereva.

Alisema kimsingi sheria inayowasimamia madereva ni ya usalama barabarani, hivyo ina kanuni zake na sheria ya wamiliki ni ya leseni za usafirishaji ya mwaka 1973 pamoja na marekebisho yote yaliyowahi kutokea.

Alisema kilichotokea ni makosa ya dereva kutoelezwa katika rasimu ya kanuni, hivyo kwa majadiliano hayo, katika rasimu ya kanuni hiyo inatakiwa kuonesha makosa yapi ya dereva na ya mmiliki wa mabasi na wakati hayo yakitekelezwa, usafiri wa abiria na mizigo nchini unaendelea kama kawaida.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Taboa, Abdallah Kiongozi alisema kiongozi wa vyama hivyo vya usafirishaji kwa pamoja wamekubaliana kusitisha mgomo na usafiri utaendelea kama kawaida.
 chanzo:habarileo.

Comments