Wafanyabiashara wakacha kukaguliwa majengo yao.

MKAGUZI wa Chakula kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Abel Deule amesema bado kuna changamoto kubwa ya wafanyabiashara kuwa na utayari wa kukaguliwa majengo yao ya biashara kutokana na wengine kukimbia wanaposikia watakaguliwa.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati wa mahojiano na kusema hali ya ukaguzi wa majengo imekuwa ikifanyika katika maeneo mengi ya mkoa wa Dodoma. 

“Bado inahitajika elimu ya kutosha ili wafanyabiashara wafahamu umuhimu wa kufanya kazi katika mazingira yasiyo salama lakini kuna changamoto kubwa kwa wahusika kukimbia wakati wanataka kukaguliwa jambo hili limekuwa likileta usumbufu,” alisema.
Alisema msindikaji wa chakula anatakiwa kuwa na kibali kinachotolewa na TFDA kabla ya kuanza kwa biashara hiyo, pia hati ya usajili wa jengo na kibali cha kutengeneza vyakula vinavyotolewa baada ya muombaji kukamilisha taratibu zote zilizoainishwa kisheria.
Deule alisema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakingalia zaidi faida na kusahau suala zima la usafi hali ambayo inahitajika kufanyika ukaguzi wa mara kwa mara na kuongeza kuwa wamekuwa wakifunga baadhi ya viwanda ambavyo havizingatii kanuni za afya ikiwemo kutokuwa na vyoo au vyoo kuwa vichafu.
Ampata mtaani mtoto wake aliyepotea MKAZI wa Ipagala Manispaa ya Dodoma, ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja juzi alifanikiwa kumpata mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 10 ambaye alitoweka nyumbani zaidi ya mwezi moja akiwa kwenye kundi kubwa la watoto wa mtaani.
Akiwa amezungukwa na kundi kubwa la watu baada ya kufanikiwa kumkamata mtoto huyo alisema, mtoto wake ni mwanafunzi wa shule ya msingi Ipagala na alitoweka nyumbani zaidi ya mwezi moja na alimtafuta bila mafanikio.
“Mimi nilikuwa nimebeba mzigo wangu natembea nasikia sauti ya mtoto akisema nisaidie fedha nikale ila ilikuwa kama sauti ya mwanangu aliyepotea nikageuka nyuma namuona mwanangu akiomba fedha kwa mpita njia aliyekuwa nyuma yangu, sikuchelewa nikamkamata mkono,” alisema.
Alisema mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu hiyo ni mara yake ya pili kutoroka nyumbani. “Watoto wa mitaani wameshamfundisha michezo mibaya ndio maana kuna wakati wenzake shuleni walikuwa wakisema hafiki shuleni anakuja mjini,” alisema.
Tukio hilo ambalo lilivutia umati mkubwa wa watu huku baadhi ya wananchi wakitaka mama huyo aondoke naye eneo la tukio. Wakizungumza jana baadhi ya wakazi wa Dodoma walisema watoto hao wamekuwa tishio kwa wapita njia kutokana na muenekano wao huku wengi wakiwa na chupa za gundi ambazo huvuta.
Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Christine Mndeme alisema itafanyika operesheni ya kuwaondoa watoto wa mitaani ambao wamekuwa kero kwa wapiti njia na wateja wanaokula hotelini ambao wamekuwa wakinyang’anywa chakula na hata vinywaji.
chanzo:Habarileo.

Comments