Watu wanne wanaotuhumiwa kufanya magendo ya bindamu wameuawa katika makabiliano na askari wa Gadi ya Pwani ya Libya.
Msemaji wa Kikosi cha Jeshi la Majini nchini Libya, Ayob Qasim amesema kuwa, makabiliano hayo yalifanyika jana Akhamisi katika mji wa Zawiya, yapata kilomita 45 magharibi mwa mji mkuu Tripoli.
Ameongeza kuwa, wafanya magendo hao wa binadamu waliagizwa kusimamisha boti yao na askari wa Gadi ya Pwani ya Libya lakini badala yake wakaanza kufyatua risasi.
Aidha mwandishi wa habari raia wa Ujerumani aliyekuwa katika manowari ya Jeshi la Majini la Libya amejeruhiwa katika makabiliano hayo ya risasi.
Itakumbukwa kuwa, Italia na Serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa yenye makao yake huko Tripoli mwezi Februari mwaka huu zilisaini hati ya maelewano kwa lengo la kutoa mafunzo, suhula na fedha za kuendeshea mapambano dhidi ya magendo ya binadamu.
Hati hiyo ya maelewano ilisainiwa kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya wakuu wa Umoja wa Ulaya huko Malta kwa shabaha ya kupambana na wahajiri kutoka Afrika kuelekea katika nchi za Ulaya.
Hivi karibuni, askari wa Gadi ya Pwani ya Libya waliwatia nguvuni wahajiri haramu 60 wenye uraia wa Bangladesh ambao walikuwa wanajaribu kuingia barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean.
chanzo:parstoday.
Comments